Nyumba 1,000 kujengwa Kawe kuboresha makazi (Ya Kimkakati)

TAASISI inayojihusisha na ujenzi wa nyumba ya Watumishi Housing Investments (WHI) imepanga kuanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba Kawe jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba mwaka huu.

Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa (WHI), Maryjane Makawia alisema jana kuwa ujenzi wa mradi huo utachukua miaka miwili hadi kukamilika kwake.

“Tumepata eneo lenye ukubwa wa ekari 10 na sasa kilichobaki ni michoro na ramani ili mradi uweze kuanza Novemba, mwaka huu,” alisema Makawia alipozungumza na HabariLEO.

Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kifungu cha 55 (h) inaeleza namna itakavyoboresha nyumba na majengo ya serikali kwa mwaka 2020-2025.

Inaeleza kuwa Watumishi Housing wataendelea kubuni na kutekeleza miradi ya kuwanufaisha watumishi wa umma, wanachama wa mifuko ya jamii na wafanyakazi wengine kwa kujenga nyumba bora na zenye gharama nafuu ambapo miradi mbalimbali imeanza kutekelezwa na mingine kukamilika.

Makawia alisema katika mradi wa Kawe wanatarajia kujenga zaidi ya nyumba 1,000 hivyo kusaidia upatikanaji wa makazi bora.

Alisema wametangaza zabuni kwa ajili ya kupata mkandarasi ambaye watashirikiana katika ujenzi wa miradi huo.

Makawia alisema WHI imepata leseni daraja la kwanza inayowaruhusu kufanya shughuli za ujenzi hivyo kwa kutumia wakandarasi wao na kampuni itakayoshinda zabuni watajenga nyumba hizo.

Alisema baada ya kupata mkandarasi watafahamu ni ajira kiasi gani zitatolewa kupitia mradi huo.

“Mkandarasi atakuja na wafanyakazi wake na sisi pia tutakuwa na wafanyakazi wetu, pia kutakuwa watu watakaojiajiri kama vile mamalishe watakaotoa huduma za vyakula kwa hiyo tutarajie ajira za kutosha kwa wazawa,” alisema Makawia.

Alisema kukamilika kwa mradi huo kutatoa fursa kwa Watanzania wataokuwa tayari kumiliki nyumba za kisasa kwa gharama nafuu.

Alisema utaratibu wa malipo utakuwa ni uleule ambao umekuwa ukitumika katika miradi yao iliyotangulia ukiwamo wa kulipia kidogokidogo wakati nyumba ikiwa kwenye ujenzi na pale itakapokamilika.

“Mteja ataweza kulipa kwa njia ya mpangaji mnunuzi au kupata mikopo ya nyumba toka benki kwa muda mrefu hadi miaka 25. Pamoja na kuuza nyumba hizi pia kutakuwa na fursa ya Watanzania kupanga kwenye nyumba hizi ndio maana kwenye mradi wetu wa Gezaulole tuna nyumba za kupanga kwenye maghorofa ili kusaidia wale ambao wanahitaji kupanga nyumba nzuri,” alisisitiza.

Mbali na mradi huo, wanategemea kuwa na mradi wa kuuza viwanja Arusha eneo la USA -River, mradi wa nyumba Dodoma katika eneo la Mtumba na Chamwino na ujenzi wa jengo la biashara Kigamboni mkoani Dar es Salaam.

Makawia alisema ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Kigamboni umekamilika hivyo Watanzania wanakaribishwa kupata maelekezo namna ya kuzimiliki.

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button