Nyumba iliyoziba geti la jirani ‘yabanwa’
NAIBU Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Juma Makungu Juma ametoa wiki moja nyumba iliyopo Fuoni Migombani ivunjwe baada ya kubainika imejengwa kinyume na utaratibu wa sheria za mipango miji na vijiji.
Agizo hilo linahusu nyumba ambayo hivi karibuni picha yake ilisambaa katika mitandao ya kijamii ikionesha nyumba inayojengwa na kuziba geti la nyumba moja inayoendelea kujengwa.
Baada ya kufanya ziara katika eneo hilo la Fuoni Jitimai Shehia ya Migombani Wilaya ya Magharibi B, alimuagiza msimamizi wa nyumba hiyo, Hafidh Ahmed Mohammed kusimamisha ujenzi sambamba na kuvunja eneo ambalo alilazimika kuweka njia.
Alisema ni vyema wananchi wakatambua umuhimu wa kuweka njia wakati wanapojenga.
“Tunapofanya taratibu za ujenzi kwanza tunapaswa kujua, hatupaswi kuziba njia ambayo inatumiwa na jamii, kufanya hivyo ni kosa na yeyote atakayekuwa anakiuka taratibu za ujenzi hatua huchukuliwa dhidi yake,” alisema Juma.
Aliwataka viongozi kushirikiana pamoja katika kutatua migogoro ya ardhi nchini ambapo mzozo huo haukupaswa kutokea endapo viongozi waliopewa dhamana ya utoaji vibali wangetimiza wajibu wao kikamilifu.
Juma alisema kwa mujibu wa sheria, anayepaswa kutoa vibali vya ujenzi ni kamati ya udhibiti na usimamizi vibali vya ujenzi (DCU) ambayo mwenyekiti wake ni Mkurugenzi Mipango miji na vijiji hivyo wananchi wanapotaka kujenga ni vyema kufika katika Taasisi hiyo iliyowekwa kisheria.
“Waliotoa vibali vya ujenzi walikuwa hawana mamlaka ya utoaji huo na hakukuwa na ufuatiliaji ndio maana yakatokea hayo na taasisi iliyopewa utoaji vibali ni (DCU), tunapaswa kulitambua hilo,” alisema.
Mkurugenzi Mipango Miji na Vijiji Kutoka Kamisheni ya Ardhi, Muchi Juma Ameir aliwataka wananchi wanapotaka vibali vya ujenzi kufika sehemu husika iliyowekwa kisheria ili kuepuka athari ambayo inaweza kutokea.
Sheha wa Shehia ya Fuoni Migombani, Kassim Abdulshakur Haji alisema atahakikisha anasimamia vyema majukumu yake hasa katika kufuatilia ujenzi unaofanywa ndani ya shehia yake kwa kila mwananchi kupaswa kuwa na kibali halali cha serikali kinachotolewa na mamlaka husika iliyopewa dhamana ya utoaji vibali vya ujenzi nchini.