Nzi wakwamisha biashara ya embe

ZANZIBAR; WIZARA ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo imesema inaendelea na utafiti wa wadudu akiwamo nzi ambao wamekuwa wakishambulia mazao ya wakulima na kurudisha nyuma juhudi za uzalishaji wa mazao ya chakula.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Mwanakwerekwe, Ameir Ali Ameir aliyetaka kujua juhudi zinazochukuliwa na wizara kupambana na wadudu hatari wanaoshambulia mazao ya wakulima.

Khamis alisema kuanzia mwaka 1990, kumejitokeza wadudu wanaoshambulia mazao ya wakulima yakiwamo maembe na machungwa, hivyo kurudisha nyuma juhudi za wakulima katika maendeleo ya kilimo na uzalishaji wake.

Kwa mfano alisema athari za nzi wanaoshambulia mazao ya kilimo yamesababisha hasara kubwa na wakulima waliokuwa wakisafirisha mazao nje ya nchi wamesita kufanya hivyo baada ya wanunuzi wa mazao hayo kupiga marufuku uingizaji wa embe hizo.

“Wakulima wa mazao ya embe waliokuwa wakisafirisha bidhaa hizo nje ya nchi lakini sasa wamesita kufanya hivyo kwa sababu ya mazao hayo kushambuliwa na kuingiliwa na nzi wanaozalisha funza,” alisema.

Alisema tayari kituo cha utafiti wa mazao ya kilimo kilichopo Kizimbani kinaendelea na kazi hiyo kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kimataifa ikiwamo kutoka Ujerumani.

Khamisi alisema mashirikiano hayo yamelenga katika kufanya utafiti wa mazao ya kilimo pamoja na mifugo ambayo yatahusisha na kujua sababu za kuwapo kwa nzi wanaoshambulia mazao.

Wazalishaji wa embe aina ya boribo katika Kijiji cha Muyuni Mkoa wa Kusini Unguja wamesitisha usafirishaji wa mazao yao baada ya nzi ambao huzalisha funza ndani ya embe kushambulia kwa wingi mazao yao na hivyo kupoteza soko la kimataifa.

Habari Zifananazo

Back to top button