TANGA: Timu ya Mkoa na Wawakilishi wa Wilaya (OCD’s) mkoani Tanga leo Januari 11, 2024 imekutana na Mwenyekiti wa Timu ya Mkoa ambaye ni Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Almachius Mchunguzi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga kwa lengo la kuwapatia semina elekezi ya namna ya kuunda Timu za Ufatiliaji wa Maekelezo yanayohusu Jeshi la Polisi kwa ngazi ya Wilaya.
Pia, Mwenyekiti wa timu ngazi ya mkoa aliwapitisha kwenye mpango wa utekelezaji wa mapendekezo ya tume ya haki jinai kwa jeshi la polisi ikiwa ni pamoja na kuwaelekeza namna ya kuchagua timu kwa ngazi ya wilaya kwa kuteuwa askari wenye weledi na uadilifu na kuwataka kuwakilisha mpango wa utekelezaji wa mapendekezo ya haki jinai kwa ngazi ya wilaya kutumwa makao makuu ya polisi.
Aidha, Kamanda Mchunguzi ameieleza timu hiyo kuwa maelekezo ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan yameanza kufanyiwa kazi na jeshi la polisi ambapo amesema maelekezo hayo ni pamoja na upatikanaji wa haki nchini ikiwa ni moja ya mapendekezo ya tume ya kuboresha mfumo wa haki jinai.
Pia,kamanda Mchunguzi amesema Rais, Dk Samia Suluhu Hassan aliunda tume kwa ajili ya kuboresha mfumo wa taasisi za haki jinai nchini.
Ameongeza kuwa Timu ya Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Maelekezo yanayohusu Jeshi la Polisi (delivery unity ), itaisaidia jeshi la polisi kuandaa mpango wa utekelezaji na utoaji wa haki kupitia mifumo iliyowekwa.