Odhiambo awatahadharisha prisons kudharau timu
KOCHA Mkuu wa Tanzania Prisons, Patrick Odhiambo leo Novemba 11, amewataka wachezaji wake kuacha kuzidharau baadhi ya timu katika Ligi Kuu Tanzania bara kwani kufanya hivyo kunaweza kufifisha malengo yao.
Akizungumza na SpotiLeo, kocha huyo amesema kipigo walichokipata jana toka kwa Coastal Union ya Tanga kimetokana na wachezaji wake kuidharau timu hiyo wakiamini haina uwezo wa kuwafunga.
“Uzembe wetu umesababisha tukapoteza pointi muhimu, wachezaji wangu wamekuwa wakizipania zaidi timu kubwa kitu ambacho kimetugarimu na kujikuta tunapoteza mchezo tukiwa nyumbani,” amesema Odhaimbo.
Kocha huyo amesema matokeo hayo yamemharibia rekodi yake nzuri aliyoanza nayo msimu huu ya kutopoteza mechi kwenye uwanja wa nyumbani wa Sokoine mkoani Mbeya baada ya awali kufungwa na Simba na jana walipoteza mchezo wa pili dhidi ya Coastal Union.
Kipigo hicho kimeiweka Prisons katika nafasi ya nane kwenye msimamo wakibakiwa na pointi zao 14 katika mechi 11 ambazo wamecheza hadi sasa kwenye ligi kuu.