Ole Sendeka aibua jambo bungeni

DODOMA; MCHANGO wa Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka kuhusu kuwepo taarifa ya Kamati Maalum inayofanya tathimini ya mapori tengefu maeneo mbalimbai nchini umezua jambo.

Akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2024/24, Mbunge Ole Sendeka, amesema kumekuwa na taarifa inasambaa mtandaoni na katika maeneo mbalimbali kuhusu kuwepo Kamati Maalum ya Wataalamu kufanya tathimini kuhusu mapori tengufu, hali ambayo imezua hofu kwa wananchi kwamba watahamishwa maeneo yao.

Hata hivyo Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki alisimama na kumpa taarifa Mbunge huyo kwamba taarifa hiyo anayoisema haipo mezani kwake na haitambui, hivyo si vizuri  kuizungumzia.

Mbunge Ole Sendeka alipoulizwa na Spika Dk Tulia Ackson kama anaipokea taarifa hiyo akasema:”Hatuwezi kupata commitment ya Mheshimiwa Waziri kuikana hiyo taarifa ili watu wapate amani maana hali ni mbaya mbaya sana. Tukishapata hiyo basi.”

Baadaye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Jenesta Mhagama alisimama kuzungumzia suala hilo na kueleza hata yeye ofisi yake haina hiyo taarifa ya Ole Sendeka.

Baada ya mjadala huo, Spika Dk Tulia alisema amepata barua kutoka kwa Ole Sendeka ambayo iliandikwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya  Simanjiro Gration Makota, inayozungumzia  tathmini ya rasilimali ya maeneo yenye wanyamapori katika mapori ya Simanjiro Belela na Simanjiro Kityangare.

Kutokana na hali hiyo Spika alimuagiza Naibu Wazuri (Tamisemi), ampigie simu Mkurugenzi huyo kumuulizia kuhusu hiyo barua iliyoandikwa kwa Ofisa Mtendaji Kijiji cha Olucholonyi Juni 19, 2023, ikielezea kuhusu tathmini ya mapori hayo..

“Waheshimiwa wabunge tuelewane kwa sababu jambo hili bado sijaweza kufanyia maamuzi kwa maelezo ninayosikia kutoka kwa Serikali, naomba tuendelee na ratiba yetu hili jambo tulipeleke mwishoni,” amesema

Habari Zifananazo

Back to top button