Ombi la Chongolo Mafinga lazaa bodaboda 16

OMBI la kupata pikipiki moja (bodaboda) lililotolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo kwa ajili ya shina namba 3K la chama hicho lililopo Mtaa wa Malingumu, Tawi la Wambi, Kata ya Boma mjini Mafinga, limezaa bodaboda 16.

Bodaboda hizo zilichangiwa baada Chongolo kuwaomba wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas na Leonard Mahenda kuchangia ununuzi wa bodaboda moja kwa ajili ya shina hilo alilolifungua leo, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya siku sita mkoani Iringa.

Wakati Asas aliahidi kununua bodaboda 10, Mahenda aliahidi mbili, Mbunge wa Mafinga Mji, Cosato Chumi moja na Katibu Mkuu mwenyewe akafunga ukurasa kwa kuahidi kuleta pikipiki tatu na hivyo kufanya jumla yake kuwa 16.

Baada ya ahadi hizo, Chongolo alishauri CCM  wilaya Mufindi kutengeneza mpango wa usimamizi wa bodaboda hizo, ili ziwe chanzo cha uhakika wa mapato ya mashina yatakayowezesha pia wenyeviti wake ambao ni mabalozi kulipwa posho ya uhakika kila mwezi.

“Idadi ya mabalozi wa CCM nchini kote ni kubwa sana. Tunajivunia mabalozi kuwa na mashina mengi nchini kote na tunatambua maombi yao posho ya kila mwezi,” alisema.

Akizungumzia ukubwa wa gharama ya kuwalipa posho mabalozi hao, alitoa mfano kwa wilaya ya Mufindi yenye mabalozi zaidi ya 2000 katika mashina yake yote akisema kama watalipwa posho ya Sh 5000 kila mwezi, chama kitahitaji kuwa na zaidi ya Sh Milioni 10 kwa wilaya moja tu kila mwezi.

Aliagiza chama hicho katika ngazi zake zote kuendelea kubuni miradi ya kiuchumi, ili kukiwezesha kumudu gharama zake mbalimbali za uendeshaji zikiwemo zile zinazohitajika na mabalozi hao.

Wakati huo huo katika ziara yake ya leo mjini Mafinga, Chongolo ameshiriki ujenzi wa shule ya msingi Muungano, amekagua barabara ya Mafinga Madibila, ametembelea kituo cha afya Ifingo na kugawa vyandarua katika tukio ambalo wanufaika wake walipewa na MNEC Salim Asas Sh 30,000 kila mmoja kwa ajili ya kununua lishe.

Aidha ametembelea mradi wa maji unaojengwa kwa zaidi ya Sh Bilioni 48, anezindua nyumba ya Katibu wa CCM na akapokea taarifa ya vibanda 33 vya biashara vya CCM  na kuvizindua kabla hajafanya mkutano mkubwa wa hadhara kuhitimisha siku ya kwanza ya ziara yake Mafinga mjini.

Habari Zifananazo

Back to top button