Ongezeko la watu lisiathiri uchumi

SERIKALI imeshauriwa kuimarisha sekta binafsi kwa kuweka mazingira yatakayovutia uwekezaji wa ndani na nje ili ongezeko la watu lisiathiri ukuaji uchumi.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi wamesema mfumo wa uchumi unahitaji mageuzi kwa kuweka sera zinazotoa kipaumbele kwa sekta zinazotengeneza ajira, kuhamasisha kilimo cha umwagiliaji, kuongeza upatikanaji wa mbolea na masoko ya bidhaa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Programu za Kumaliza Umaskini (REPOA), Dk Donald Mmari alisema sekta binafsi ndio ina wigo mpana wa kuingiza vijana kupata ajira hivyo wanahitaji elimu bora inayowapa ujuzi katika kuzalisha na kufanya kazi zao kwa tija kulingana na ujuzi wanaopata.

Dk Mmari alisema asilimia 60 ya Watanzania wote nchini ni vijana chini ya miaka 24, hivyo lazima kuwa na mifumo itakayowaandaa kuingia kwenye shughuli za uzalishaji. “Mifumo yetu inahitaji kuzipa kipaumbele sekta zenye uzalishaji zaidi ziwe na tija kwa rasilimali zilizopo zibadilishwe na kuwa bidhaa hivyo mnyororo wa thamani utaonekana na ndipo vijana watapata ajira,” alisema.

Pia Dk Mmari alisema sekta zinazohitajika zaidi ni zile zinazoongeza mnyororo wa thamani ikiwamo viwanda hivyo kuchochea ongezeko la ajira na uzalishaji kwa rasilimali zilizopo.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Lawi Yohana alisema ongezeko la watu lina athari chanya katika ukuaji wa uchumi kwa sababu asilimia kubwa ya watu waliopo ni vijana. Dk Yohana alisema ili uchumi uendane na ongezeko la watu na kuleta manufaa ni lazima kufungua fursa zaidi za kilimo kwa kuhamasisha kilimo cha umwagiliaji, kuongeza upatikanaji wa mbolea na masoko ya mazao.

Mchambuzi wa uchumi, Profesa Humphrey Moshi alisema uchumi wa Tanzania umekua kwa asilimia 5.4 wakati ongezeko la watu lipo katika asilimia 3.

2 kwa mwaka hivyo ili uchumi ukue ni lazima ufikie asilimia nane na kuendelea. Profesa Moshi alisema msichana akipata elimu ana uwezo wa kupanga idadi ya watoto anaowahitaji katika familia yake, na hawataweza kuwa na watoto saba au zaidi.

“Mtoto wa kike anapomaliza chuo kikuu atakuwa na miaka 25 ambapo atakuwa na elimu kuhusu masuala ya afya ya uzazi, ataweza kujadiliana na mwenza wake idadi ya watoto wanaowataka na kuhakikisha watoto waliopanga wanapata elimu bora, afya bora na kuhakikisha ustawi wa maisha yao,” alisema.

Aliongeza: “Ukitaka kuboresha maisha ya watu kwa haraka ni lazima uhakikishe uchumi unakua zaidi ya idadi ya watu, kutokana na majanga ya Covid-19 na vita kati ya Ukraine na Urusi nchi haiwezi kulaumiwa, lakini ongezeko la asilimia 3.2 ni alama mbaya katika ukuaji wa uchumi wetu.”

Alisema kundi kubwa la watu wenye umri wa miaka 25 hadi 60 linaashiria uwepo wa nguvu kazi ya kutosha yenye tija kusaidia makundi tegemezi ya watoto na wazee.

“Angalizo, kama nguvu kazi hii kubwa haina ajira, ni tatizo hivyo ni lazima kuhakikisha nguvu kazi hiyo wanapata mahitaji ya elimu bora na afya bora ili kuwa na nguvu kazi yenye afya na itakayoongeza uzalishaji wenye tija,” alisema Profesa Moshi.

Habari Zifananazo

Back to top button