Ongezeko ugonjwa wa kisukari, watakiwa kuzingatia haya
DAR ES SALAAM; IKIWA jana ni siku ya ugonjwa wa kisukari Duniani takwimu zinaonesha wagonjwa wa kisukari wameendelea kuongezeka nchini huku utafiti mpya ukisubiriwa mwishoni mwa mwaka huu.
Hayo yamesemwa katika maadhimisho ya wiki ya magonjwa yasiyoambukiza yanayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam na Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti na Kuzuia magonjwa yasiyoambukiza, Valeria Mlinga.
Mlinga amesema kwa kipindi cha kabla ya miaka 30 kati ya watu 100 mtu mmoja alikuwa na kisukari lakini sasa katika 100 watu tisa wanakutwa na kisukari kwa utafiti uliofanyika miaka 11 iliyopita.
Aidha ameongeza kuwa takwimu za vituo vya afya zinaonesha kuwa mwaka 2017 wagonjwa waliotibiwa magonjwa yasiyoambukiza walikuwa milioni 2.5 na mwaka 2021 waliongezeka hadi milioni 3.
4 sawa na ongezeko la asilimia 9.4.
“Lakini sasa tunafanya utafiti kuhusu ugonjwa wa kisukari na mengine tutapata matokeo mwishoni mwa mwaka huu au mwakani mwanzoni itatupa picha halisi
Amesema magonjwa yasiyoambukiza hapa nchini yanachangia vifo kwa asilimia 33 ambapo kati ya watu 100 watu 33 hupoteza maisha.
“Na kila mwaka tunafanya maadhimisho ya wiki ya kuzuia na kudhibiti magonywa hayo lengo ni kuleta uelewa na hamasa kwenye jamii namna ya kujikinga na jamii inatakiwa kutambua sababu ya ongezeko la magonjwa hayo.
Ameyataja Magonjwa hayo kuwa ni shinikizo la juu la damu,kisukari,saratani ,magonjwa afya ya kinywa na meno,macho na magonjwa ya akili.
Mlinga amesema kwa mwaka huu madhimisho yanafanyika Mkoa wa Dar es Salaam ambapo Novemba 11 walianza na matembezi ya watu wenye umri mkubwa na yatahimishwa Novemba 18 ,2023.
“Lengo ni kuonesha tunawajali,tunawapenda na mara nyingi matembezi mengi yamekuwa na vijana lakini wazee wanaathirika.
Amesema katika wiki hiyo wanafanya uchunguzi wa afya bure,upimaji wa macho na utoaji miwani bure na upimaji meno na kupewa miswaki na dawa za meno na dawa zitatolewa pia.
Ametaja kuwa mabadiliko ya mtindo wa maisha yanasababisha ongezeko la magonjwa hayo ,watu kutofanya mazoezi,ulaji mbaya wa vyakula kama sukari nyingi na mafuta huku mazoezi yakifanyika kwa kiasia kidogo.