‘Ongezeni kasi unenepeshaji ng’ombe kuna soko kubwa’

RAIS Samia Suluhu amewataka vijana wanaoshiriki programu ya Jenga kesho iliyo Bora (BBT),kuongeza kasi ya unenepeshaji wa ng’ombe kutokana na kuwepo kwa soko kubwa la nyama ndani na nje ya nchi.

Rais Samia ametoa wito huo leo Agosti 8,2023 alipotembelea banda la unenepeshaji wa ng’ombe kupitia programu hiyo lililopo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi,kwenye maonesho ya Nanenane viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya.

“Wanangu soko la nyama ni kubwa mno hata wanyama hai kuna kipindi nchi za wenzetu huko wanataka, sasa wanyama wakuja kuwachukua ni hawa walioko kwenye mabanda yetu, lakini pia tuna soko ambalo hatuwezi kulisha mpaka nilizungumza na Waziri wa Zambia nikamwambia tuletee tuchanganye tupeleke kwa pamoja, ili Tanzania isikose hilo soko,”amesema Rais Samia.

Advertisement

Amesema wapo vijana wengi wakiwemo waliohitimu mafunzo ya JKT hawana kazi, hivyo programu hiyo ikihamasishwa itawezesha vijana wengi kujiajiri na kuongeza kipato chao na Taifa kwa ujumla na kuwataka vijana wanaoshiriki programu hiyo kutokata tamaa kutokana na changamoto wanazokabiliana nazo wanapotekeleza programu hiyo.

Amewapongeza wataalamu wa mifugo kwa kusimamia vizuri programu hiyo na kufanikisha maendeleo yaliyopatikana hadi sasa .

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega amesema programu hiyo imeleta mafanikio makubwa ambapo kampuni ya Heifer International imeunga mkono kwa kuwaunganisha na wadau wa vyombo vya habari vya mitandaoni kwa lengo la kuwawezesha vijana wanaonenepesha ng’ombe kuuza kwa njia ya mtandao.

Waziri Ulega ameongeza kuwa tayari Wizara ya Fedha imeanza mipango ya wa kuwaingiza vijana hao katika masoko ya kimtandao, badala ya kutegemea masoko ya minada ya vijijini, ili kuwasaidia kupata masoko ya kimataifa.

“Tumezungumza pia na benki yetu ya maendeleo ya kilimo TADB pamoja na benki nyingine ziamini katika ufugaji huu wa unenepeshaji mifugo,na kuanza kuwakopesha vijana wetu, Ili wapate mitaji,”amesema Waziri Ulega.

Mmoja wa wanufaika wa unenepeshaji ng’ombe Rest Gonja ,amesema hadi sasa programu hiyo imewaingizia faida ya zaidi ya Sh Millioni 74 kutokana na ng’ombe 655 waliowauza kati ya ng’ombe 2400 waliowanenepesha.

6 comments

Comments are closed.