Onyo latolewa wanaochelewesha miundombinu ya shule

MOROGORO: KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ,Adolf Ndunguru amewataka viongozi wa mikoa na halmashauri ambazo ujenzi wa miundombinu ya shule haijakamilika wajitafakari wenyewe kabla ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Ndunguru ,amesema hayo Januari 4, 2024 wakati akifungua kikao kazi cha Makatibu Tawala wasaidizi elimu mikoa na maofisa elimu wa halmashauri nchini mjini Morogoro
Aidha amesema pamoja na dhamira njema ya serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya elimu, wapo baadhi ya viongozi ambao wameshindwa kusimamia na kukamilisha utekelezaji wa miradi hiyo kwa muda uliopangwa .
Katibu mkuu huyo alitolea mfano kuwa ,ipo mikoa ambayo ujenzi wa miundombinu ya shule bado ipo chini ya asilimia 50, licha ya maelekezo ya serikali ya kuwataka kukamilisha ujenzi kabla ya Desemba 30, 2023.
Ndunguru ,ameongeza kumekuwepo na visingizo na maelezo luluki kuhusu changamoto za kutokamilisha kazi hiyo na sababu hizo haziwezi kusaidia kwa wakati huu .
“ Kumbukeni kuwa wapo wenzenu wamekamilisha miradi hiyo huku wakiwa na mazingira magumu kuliko nyie mnaosuasua “amesema Ndunguru.