Oparesheni uhalifu yanasa silaha 997

JUMLA ya silaha 997 zimekamatwa kutokana na oparesheni mbalimbali za kuzuia na kutanzua uhalifu mkoani Morogoro kuanzia Januari mwaka 2019 hadi Juni mwaka huu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilimu alisema hayo juzi katika taarifa yake kwa mkuu wa mkoa huo, Fatma Mwasa. Alisema silaha hizo zilikamatwa kupitia Kitengo cha Usimamizi na Udhibiti wa silaha.

Mwasa alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa warsha ya kuwajengea uwezo viongozi na watendaji wa makundi mbalimbali ya kijamii na serikali mkoani humo kuhusu mwezi wa usalimishaji silaha haramu Afrika ambayo iliandaliwa na jeshi hilo.

Musilimu alisema katika kipindi hicho jumla ya silaha 52 zilizokuwa zinamilikiwa kihalali ziliporwa kutoka kwa wamiliki na kuangukia kwenye mikono ya watu wasio wazuri.

Alisema Tanzania ni mwanachama na imesaini mikataba mbalimbali ya kimataifa na ya kikanda ya kupambana na suala la uzagaaji wa silaha haramu. Pia imeingia makubaliano na Umoja wa Afrika ya kuondoa silaha haramu kwa kutangaza Septemba kuwa ni mwezi wa msamaha kwa kusalimisha silaha haramu.

Makubaliano hayo ni ya kuanzia mwaka 2017 hadi 2030. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Septemba 5, mwaka huu alizindua kampeni ya usalimishaji wa silaha kwa hiari jijini Dodoma na kutangaza kazi hiyo kuwa ilianza Septemba Mosi mwaka huu na kuendelea hadi Oktoba 31, mwaka huu.

Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi na Udhibiti wa Silaha Makao makuu ya Polisi Dodoma, Rienada Millanzi alisema kwa mara ya kwanza, nchi ilitangaza msamaha wa usalimishaji wa silaha haramu Novemba, mwaka 2021 na silaha haramu 228 zilisalimishwa.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Fatma, katika hotuba ya ufunguzi alisema kuwa takribani asilimia 80 ya matukio ya uhalifu yanafanyika kwa kutumia silaha ambazo hazimilikiwi kihalali.

Habari Zifananazo

Back to top button