Operesheni funga maduka yazua gumzo Bukoba, Machali acharuka

MKUU wa Wilaya ya Bukoba, Mosses Machali ameelekeza maduka yote ya wafanyabiashara ambao hawana leseni za biashara yafungwe hadi hapo watakapopata leseni ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Operesheni Funga Maduka.

Machali amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Hamid Njovu wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani waliokuwa na hisia tofauti wakati wakipitia ripoti ya kwanza ya mwaka wa Fedha 2022/23. Ripoti hiyo iliyowasilishwa na Mstahiki Meya, Godson Gipson pia ilihusishwa operesheni ya kufungia maduka ya wafanyabiashara katika Manispaa ya Bukoba. Kikao hicho kimedumu kwa zaidi ya saa 9.

Kwa mujibu wa Msitahiki Meya, Kanuni za Baraza la madiwani zinasema kuwa kupitia Baraza la madiwani  kamati ya Fedha inapaswa kuletewa majina ya wafanyabiashara  wadaiwa sugu na wafanyabiashara hao wanapaswa kuitwa na kuhojiwa na baada ya kushindikana kulipia Leseni na sehemu zakutolea huduma wafanyabiashara hao wanapaswa kupelekwa mahakamani na sio Kufunga maduka yao.

“Zoezi limefanyika lakini halikufuata utaratibu,” amesema Gipson. “Hakuna Diwani anayepinga mapato yasikusanywe, hakuna anayepinga wafanyabiashara kuwajibishwa lakini hapa tunachopinga hii operesheni ya Kufunga maduka imeleta kero kwani kikosi kazi kilichoundwa hakitoi nafasi ya kumusikiliza mfanyabiashara.”

Gipson amedai kwa kikosi kazi hicho kimekuwa kikifunga maduka ni kama mamlaka tofauti inayoingilia mamlaka nyingine.

Baadhi ya madiwani akiwemo Diwani wa kata Bakoba Shabani Rashidi na Diwani wa kata Bilele Tawfiq Sharif  kupitia Baraza hilo wakamuomba mkurugenzi kutoa siku 30 kwa wafanyabiashara hao ili waweze kulipia Leseni na wengine kusajili Biashara zao.

Wafanyabiashara hao pia wanahusisha wale ambao waliwahi kutumia vitambulisho vya elfu 20,000 na baada  ya muda wa vitambulisho hivyo kuisha hawakupewa muda mwingine wa kuelimishwa au kutafuta Leseni za Biashara.

Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Bukoba alipinga nyongeza ya muda na kumuagiza Mkurugenzi kuwa zoezi la kukagua Leseni na Kufunga maduka liendelee katika mitaa yote 66 ya Manispaa ya Bukoba. Amesema taaarifa za kiintelejensia zimebaini kuwa baadhi ya Wafanyabiashara hawajalipia Leseni zaidi ya miaka 2 na wana elimu ya kutosha kuhusu Biashara.

“Sita kubari hata kidogo swala la Biashara ni swala nyeti naomba niwape taarifa kidogo hii operesheni ya siku 10 imefanya ukaguzi na kugundua wafanyabiashara wana leseni hawajawai kulipa hata kidogo, wengine wanamaduka makubwa hawana Leseni,” amesema. “Lakini pia robo ya kwanza ya mwaka wa Fedha 2022/2023 hatukutimiza malengo ya kukusanya tumekusanya asilimia 25 badala ya asilimia 30 je hizi fedha walizokalia wafanyabiashara si zingetimiza lengo,” alihoji Machali.

Alitoa wito kwa wanasiasa kuacha kujiingiza katika mgongo wa kutetea wafanyabiashara wasiotaka kulipa Kodi kwani Halmashauri ikifutwa nao hawatakuwa na nafasi za uwakilishi kwa wananchi wao lakini pia watakosa posho mbalimbali zilizowekwa kisheria endapo Halmashauri ikikosa mapato.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Hamid Njovu akitoa taarifa ya Operesheni katika kata 4 zilizofikiwa amesema kuwa zaidi ya Wafanyabiashara 400 hawakuwa na Leseni, zaidi ya Wafanyabiashara 600 hawakulipa Leseni zao muda ulipita na ndani ya siku kumi tangu zoezi Hilo kufanyika tayari wafanyabiashara wamelipia zaidi ya Sh milioni 103 na waliolipia maduka yao yamefunguliwa.

Alitoa wito kwa madiwani kuwa Kama wanataka maendeleo ndani ya Halmashauri yao ni vyema washiriki kutoa Elimu kwa wafanyabiashara wao huko mtaani na kuendelea kushikamana pamoja ili watimize lengo la kuiendesha Halmashauri pamoja bila kukwazana huku kila mmoja akitimiza wajibu wake.

 

Habari Zifananazo

Back to top button