Osimhen kuishtaki Napoli
WAKALA wa mshambuliaji Victor Osimhen wa Napoli, Roberto Calenda ametishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya klabu hiyo baada ya kumkejeli mshambuliaji huyo kwenye mitandao ya kijamii.
Napoli walichapisha video kwenye akaunti yao ya TikTok ikimuonesha mshambuliaji huyo akikosa penalti dhidi ya Bologna, na sauti ya juu ikisema ”gimme penalty please”.
Hata hivyo Napoli wameifuta video hiyo lakini ilikuwa imeshawafikia watu wengi na tayari ipo mitandaoni, kitu ambacho Victor inasemekana hajakipenda.
“Tunahifadhi haki ya kuchukua hatua za kisheria na mpango wowote muhimu wa kumlinda Victor,” Calenda aliandika kwenye X.
“Kilichotokea leo kwenye wasifu rasmi wa Napoli kwenye jukwaa la TikTok hakikubaliki.
” Aliongeza.
Osimhen alionekana akimhoji meneja Rudi Garcia alipotolewa nje dakika ya 86 katika mchezo wa Jumapili dhidi ya Bologna.
Mchezaji wa kimataifa wa Nigeria Osimhen alijiunga na Napoli kwa rekodi ya Euro milioni 81.3 katika msimu wa joto wa 2020 na aliwasaidia kushinda taji la kwanza la Serie A katika miaka 33 msimu uliopita, akifunga mabao 26 katika mechi 32 za ligi.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 – ambaye alihusishwa na Chelsea na Manchester United msimu huu wa joto – amefunga mabao matatu katika mechi sita msimu huu.