OUT kuna mambo mazuri kwa walimu

OUT kuna mambo mazuri kwa walimu

CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), kinatoa mafunzo ya ualimu kwa walimu wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, ili kuwajengea uwezo wa kuwapatia mbinu za ufundishaji na ujifunzaji walimu wa fani hiyo, huku wakiendelea na kazi zao.

Makamu Mkuu wa OUT, Profesa Elifas Bisanda amesema hayo alipotembelea maonesho ya Baraza la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) yanayoendelea jijini Arusha.

Profesa Bisanda amesema OUT kwa kushirikiana na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi (VETA) Morogoro kinatoa program inayoitwa  “Postgraduate Diploma in Technical and Vocational Teacher Education (PGD-TVTE) kwa wahandisi wenye shahada ambao ni walimu katika vyuo vya ufundi.

Advertisement

“Programu hii ni nzuri sana kwani huwawezesha wahandisi na wengine wote wanaofundisha katika vyuo vya ufundi kuwa na ujuzi wa mbinu za ufundishaji na ujifunzaji pamoja na ubunifu unaosadia kuzalisha mafundi wabobezi katika fani zao hapa nchini,” amesema.

Amewataka wahandisi na watu wa fani nyingine ambao ni walimu wa ufundi au wanatarajia kuwa walimu wa fani za ufundi kujiunga na programu hiyo, ambayo inawapatia fursa ya kusoma wakiwa wanaendelea na kazi zao popote pale walipo.

“Kozi hii hufunzwa kwa mwaka mmoja wa masomo na maombi yanapokelewa kupitia www.out.ac.tz au fika kwenye kituo cha karibu cha OUT ujaze fomu,”amesema.