OUT, VETA wazindua programu ya uzamili

CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwa kushikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), imezindua Program maalum ya stashahada ya uzamili katika ualimu wa ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

Akizindua kozi hiyo Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk Wilson Mahera amesema program hiyo imezinduliwa wakati muafaka kwa kuwa itakidhi mahitaji.

Amesema uzinduzi huo wa program hiyo ni wa kipekee kwa kuwa OUT kitatoa zaidi mafunzo ilhali VETA watatumia karakana zao kuhakikisha wanafunzi wanaiva ipasavyo.

“Ili nchi ifikie malengo yake ya kimaendeleo ni lazima uwekezaji kwa upande wa sayansi na tekknolojia upewe kipaumbele.

” Hivyo waalimu hawa wanapopata mafunzo haya watakuwa na umahiri mkubwa zaidi katika kutoa elimu hizi za sayansi na teknolojia ili kuendana na utekelezaji wa dira ya maendeleo ya nchi ya mwaka 2025 ambayo inataka wananchi wakitoka kwenye elimu waweze kukabiliana na changamoto za kimaisha na kuzishinda.” amesema.

Makamu Mkuu wa OUT, Profesa Elifas Bisanda, amesema mafunzo hayo yanaendeshwa kwa kutumia zaidi Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kumfanya mwanafunzi aweze kumaliza kwa muda mfupi.

Pia kumwezesha asome akiwa kazini akiendelea kutimiza majukumu yake ya kikazi.

“Mafunzo haya tunaamini yatakuwa ufunguo wa kuhakikisha kuwa wataalam wa fani mbalimbali za ufundi wanaboreshwa na kuwezeshwa kufundisha kwa ustadi ili kwenda kuzalisha watu ambao watakuwa na nguvukazi ya kutosha katika ufundi.” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore, amesema lengo kuu la muunganiko huo ni kushirikiana katika kutoa elimu pamoja na kuhakikisha kuwa serikali inafikia malengo yake ya kuwa na walimu wa kutosha.

“Ushirikiano huu umeweza kutujenga zaidi katika kuimarisha uzoefu tunaobadilishana kupitia utoaji wa haya mafunzo na matunda yameanza kuonekana.

“Sote tunajenga nyumba moja hivyo tunataraji kujiimarisha zaidi ili kuhakikisha kuwa wigo wa upatikanaji wa waalimu nchini ambao wanakuwa na ujuzi na uelewa katika elimu ya ufundi na ufundi stadi nchini unaongezeka,” amesema.

Kozi ya Stashahada ya Uzamili katika Mafunzo ya Ufundi na Ufundi Stadi ambayo ilipata ithibati yake mwaka 2020, inatolewa kwa pamoja kwa kushirikiana baina ya OUT na VETA ili kutoa taaluma ya ualimu kwa waalimu wa ufundi na ufundi stadi ili kuwapa umahiri katika ufundishaji.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button