PAC yaridhishwa mradi wa maji Butimba

MWANZA: KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeridhishwa na ufanisi wa mtambo wa kuzalisha na kutibu maji wa Butimba Mkoani Mwanza na imepongeza jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kufanikisha mradi huo.

“Kwa tulichokiona kinavutia sana na kinafurahisha, tumeanzia pale maji yanapochotwa ziwani hadi hatua ya mwisho ambapo majisafi na salama yanaruhusiwa kufika kwa wananchi kwa tulichokiona kwa macho ni kitu kizuri, ni mradi mzuri,” amesema Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Japhet Hasunga mara baada ya kutembelelea na kukagua mradi huo.

Amebainisha lengo la ziara ya Kamati katika mradi huo ni kushuhudia uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali na kutazama namna ambavyo fedha ya umma inavyotumika katika utekelezaji wa miradi.

Mwakilishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Ellen Bogohe ameshukuru Kamati kwa kutembelea mradi huo ambao amesema ni wakipekee kuwahi kujengwa Nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Neli Msuya ameelezea hali halisi ya uzalishaji maji na mahitaji yaliyopo pamoja na mipango inayoendelea kutekelezwa na serikali.

Amesema mradi umekamilika kwa asilimia 100 na uzalishaji unafanyika kulingana na usambazaji unavyokwenda na kwamba hatua zinazoendelea ni kuboresha mifumo ya usambazaji maji, ili kufikia wananchi wengi zaidi kadri ambavyo mradi ulivyotarajiwa kufika.

 

Habari Zifananazo

Back to top button