Pacha walioungana Tabora wahamishiwa Saudi Arabia

MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Mohammed Janabi amesema kitendo cha Saudi Arabia kuamua kuwahudumia watoto pacha walioungana Hassan na Hussein kinaashiria mahusiano mema na adhimu kati ya Tanzania na nchi hiyo.

Profesa Janabi amesema hayo Dar es Salaam leo wakati Kaimu Balozi wa Saudi Arabia nchini Fahad Alharbi alipokwenda kuwajulia hali watoto hao, ambao wamekuwa wakipatiwa matibabu kwa takribani miaka miwili sasa.

Balozi huyo aliwasili Hospitali ya Taifa Muhimbili kuwajulia hali watoto mapacha Hassan na Hussein ambao wameungana sehemu ya kifua, tumbo na nyonga na wana miguu mitatu wako hospitalini hapo pamoja na Mama yao.

Akizungumza na waandishi wa habari, Profesa Janabi alisema kitendo cha Saudi Arabia kuwatibu kwa kuwapeleka nchini kwao ni ishara ya uhusiano mwema uliopo.

Amesema ana matumaini kuwa matibabu ya watoto hao yatafanikiwa kutokana na mafanikio waliyonayo Saudi Arabia katika sekta ya afya.

Naye, daktari Bingwa wa upasuaji wa watoto, Zaituni Bokhary alisema watoto hao wataambatana na jopo la wataalam kwenda Saudi Arabia kimatibabu.

Watoto mapacha Hassan na Hussein  wenye mwaka mmoja na miezi 11 walipelekwa Muhimbili wakiwa na wiki mbili wakitokea Tabora, ambapo wanatarajiwa kusafiri kesho kwenda Saudi Arabia kwa ajili ya matibabu zaidi.

Habari Zifananazo

8 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button