PADRI wa Kanisa Kuu la St. Joseph Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Gasper Basilidi amesema moja ya sababu zinazochangia kushamiri kwa biashara ya binadamu ni ongezeko la pengo baina ya walio nacho wasionacho.
Utofauti huo, kwa mujibu wa Padri Basilidi, unatumika kama mwanya kukandamiza na kudhalilisha utu wa mwanadamu.
Basilidi alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati akielezea harakati za upingaji wa biashara haramu ya binadamu.
Alisema biashara hiyo inakinzana na uumbaji wa Mwenyezi Mungu hivyo ni vyema kuipinga kwa nguvu zote.
“Hatuwezi kufanana tumeumbwa tofauti, tumezaliwa tofauti, tunaishi tofauti na tutazikwa tofauti ndio sababu ya sisi kutegemeana na kusaidiana kweli na sio kinyume chake,” alisema.
Alisema ili kupinga kitendo hicho cha biashara haramu ya binadamu, wameandaa filamu ijulikanayo kama ‘utu’ ili kupaza sauti wengi wajue ubaya wa biashara hiyo.
Kwa upande wake Mohamed Nzunda ‘Mkojani’ alisema ameungana na Kanisa Katoliki katika kampeni ya kukemea biashara hiyo haramu ya unyanyasaji na uuzaji wa binadamu kwa kushiriki filamu hiyo ya utu.
“Sinema hii inaelimisha watu ambao wanadhani wanaishi kama wanawasaidia wengine kumbe wanawatumia vibaya, kuna watu wanafanyishwa hiyo biashara ya kuuzwa lakini wanakuwa
wanawashukuru wale mabosi bila kujua,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Kanda ya Mashariki katika Kampeni hiyo ya kupinga usafirishwaji haramu wa binadamu, Baptista Nzunda alisema wamekuwa wakifanya miradi mbalimbali ukiwemo huo wa
kutokomeza biashara hiyo haramu.
Alisema mradi huo umezindua filamu itakayotoa mafundisho na uelewa katika jamii ya Kitanzania.