DAR ES SALAAM: KILA ifikapo Desemba 26 ya kila mwaka, waumini wengi wa dini ya kikristo wa madhehebu mbalimbali hutumia siku hii kwaajili ya kufungua zawadi walizotunukiana baina yao katika siku ya Krismasi.
Kimombo siku hii hutambulika kama ‘Boxing Day’.
Kubaini namna wanavyosherehekea siku hii, tumezungumza na waumini mbalimbali wa Dini ya Kikristo wa jijini Dar es Salaam kupata kufahamu namna wanavyoielewa siku hii na namna wanavyoiadhimisha na kuisherehekea.
“Ninavyofahamu kuhusu Boxing Day, ni ole siku ya kupeana zawadi,” amenukuliwa Neema Noel, Muumini wa Dini ya Kikristo na mkazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Adolf Mkwinyo naye ni muumini wa Dini ya Kikristo ila ana mawazo kinzani na wale wanaoona Boxing Day kama siku ya masumbwi.
“Boxing Day ni kiingereza, maana yake ni siku ya kufungua zawadi wala sio mapambano kama wengine wanavyoichukulia,” amesema Mkwinyo.
Naye, Joshua Isac mfanyabiashara wa bidhaa za kikristo nje ya geti la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Azania Front, Posta Dar es Salaam anasema kupeana zawadi ni ishara ya upendo.
“Wakati mwingine mahusiano hujengwa kupitia zawadi. Nimeshuhudia kadhaa wakifunga ndoa, kupitia siku hii,” amesema Jonas.
Ili kupata ufahamu zaidi juu ya siku hii, tumezungumza na Padri kutoka kanisa la Katoliki Jimbo Kuu la Tabora, Leons Maziku.
Anatueleza historia ya kuadhimisha siku hii kuwa ilianza tangu kale ambapo Wakristo matajiri wakati wakusherehekea sikukuu ya Krismasi walikuwa wakipeana maboksi ya zawadi.
“Na walikuwa wakitumia siku hii kupumzika na kufungua maboksi ya zawadi zao,” amesema Father Maziku.
Aidha, kiongozi huyo amekemea upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu kwa kutumia siku hii kufanya vurugu, kulewa na mambo mengine maovu.
“‘This is wrong’. Ni upotoshaji kabisa, siku hii haihusiani na jinai yoyote, na hata wanaohusianisha na mchezo wa masumbwi, mbona hata mchezo huo una taratibu zake?.” Amehoji kiongozi huyo.
Hata hivyo, kiongozi huyo amewataka waumini wa Kikristo na watu wengine kutotumia kigezo cha siku hii kwa kufanya jinai.
Comments are closed.