MAMIA ya waumini wa Kanisa Katoliki wamehudhuria kusimikwa Padri Christopher Nkoronko kuwa Askofu Jimbo Katoliki Kahama.
Askofu huyo aliteuliwa na Baba Mtakatifu, Francisko kushika nafasi hiyo tangu Machi 19, mwaka huu.
Askofu Mkuu, Paul Ruzoka wa jimbo kuu la Tabora aliyeendesha ibada ya uwekaji wakfu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Karoli Lwanga alisema ngazi ya uaskofu ina kazi kubwa kwani inahitaji kutimiza mapenzi ya Mungu.
Askofu Mkuu Ruzoka alisema Christopher Nkoronko ameteuliwa nafasi hiyo ya Askofu aitumikie vyema bila ubaguzi nakutafuta kondoo waliopotea.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan alimpongeza Askofu Nkoronko kwa kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye alisema wananchi wa Kahama wamepata mtu makini na mwenye upendo apate ushirikiano kwa wananchi wote.
Andengenye alisema kuwa kazi nzuri aliionesha tangu awali akiwa mkoani Kigoma hivyo aendelee kutenda mema .
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Festo Kiswaga alisema kuwa amefurahi kuona maelfu ya watu kuja kumpokea Askofu Nkoronko.