SERIKALI imefanikiwa kudhibiti wimbi la uhalifu jijini Dar es Salaam, maarufu kama panya road na sasa hali ni shwari ikilinganishwa na ilivyokuwa hapo awali.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema hayo Jumatano mjini Moshi mkoani Kilimanjaro wakati wa maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani yenye kaulimbiu “Amani yetu maendeleo yetu”.
Majaliwa alisema uchunguzi wa awali umebainisha wahalifu hao ni kikundi cha vijana kilichotoka kutumikia kifungo gerezani ambacho kimeungana kwa lengo la kuleta uhalifu.
“Serikali itafanya jitihada mbalimbali kulinda amani, hivi karibuni pale Dar es Salaam, kilijitokeza kikundi cha wahalifu waliokuwa magereza, wanataka kurudi tena gerezani kwa kufanya uhalifu, tumewadhibiti,” alisema.
Aliongeza: “Najua Kilimanjaro vikundi hivi havipo lakini siyo jambo jema, ninyi wakuu wa wilaya na mikoa ndiyo maana mmepewa cheo kingine cha uenyekiti wa kamati ya usalama ya wilaya au mkoa, dhibitini viashiria vyovyote.”
Alitaka viongozi hao kuingia maeneo yoyote kwa kutumia wadhifa walizonazo ili kudhibiti viashiria vyovyote ambavyo kwa namna moja au nyingine vinakwenda kuvuruga amani iliyopo.
Alisema vyombo vya ulinzi na usalama vinafanyakazi kubwa na serikali itaendelea kuenzi kazi hiyo ili Taifa liendelee kuwa salama.
Aidha, waziri mkuu alisema serikali inathamini juhudi za makundi yote yenye lengo la kulinda amani iliyopo nchini na kwamba serikali itazidi kutoa ushirikiano wake.