Panya Ronin akaribia kumfunika Magawa
CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimesema panya dume aliyepewa jina la Ronin anafanya kazi nzuri kutafuta mabomu na vilipuzi nchini Cambodia na uwezo wake unakaribia kumzidi mtanguliz wake, Magawa.
Ofisa Mawasiliano wa Mradi wa Apopo SUA mkoani Morogoro, Humphhrey Makusa amesema Ronin alizaliwa Augosti 13, 2019 na ana uzito wa kilo 1.5.
Makusa alisema hayo kwenye kituo cha mradi huo kilichopo chuoni hapo na akabainisha kuwa Ronin alipelekwa Cambodia Machi 6 mwaka 2021 baada ya kufuzu mtihani.
Kupitia mradi huo, SUA wanafanya utafiti na kuwafundisha panya namna ya kutafuta mabomu yalitotegwa ardhini na vilipuzi na wanaofuzu wanasafirishwa kwenda kufanya kazi katika maeneo yaliyoathiriwa ikiwamo Cambodia.
Makusa alisema kituo hicho kinafanya utafiti wa panya na kutoa mafunzo na hadi sasa kina panya wasipungua 164 na 64 kati ya hao wapo kwenye mafunzo ili wakafanye kazi ya kuonesha mabomu.
Panya Magawa alifuzu mitihani mwaka 2016 akapelekwa kufanya kazi ya kutafuta mabomu na vilipuzi nchini Cambodia.
Magawa alisifika kusaidia kugunduliwa kwa zaidi ya mabomu 108 ya kutegwa ardhini nchini Cambodia.
Septemba 2020, Shirika lisilo la kiserikali la Matibabu ya Wanyama la Uingereza (PDSA) lilimtuza panya Magawa medali ya dhahabu kutokana na ushujaa na kujitolea kuokoa maisha ya watu nchini Cambodia.
Magawa alistaafu mwaka 2021 na baada ya hapo kituo cha Apopo kilipeleka panya wengine 45 nchini humo akiwamo Ronin.
Makusa alisema, Ronin alifundishwa kwa mwaka mmoja na alianza kufanya kazi Machi 6, 2021 na hadi sasa juhudi zake zinakaribia kumpita Magawa.
Mkufunzi wa panya katika kituo hicho, Abouswai Msuya alisema kwa zaidi ya miaka 30 wamefundisha panya kugundua mabomu yaliyotengwa ardhini.
Msuya alisema mafunzo huanza wakati panya ana umri wa wiki nne kwa kuwaweka katika mazingira ya kuishi na binadamu ili kuwatoa uoga na hofu wanapoona binadamu na mazingira mapya.
Alisema panya hao wanafundishwa kusikia mlio fulani ambao unaashiria kuna chakula kimewekwa mahala na pia hufundishwa kutofautisha harufu ya mabomu hayo ya chini ya ardhi ya TNT na harufu nyingine.
“Panya hawa tunao wafundisha wanaweza kugundua mabomu hata yakiwa yamekaa kwa miaka 30 ardhini,” alisema Msuya na akasema panya waliopata mafunzo hayo wamefanya kazi Msumbiji na sasa wapo Angola na Cambodia.