PANYA wameteketeza alizeti na mahindi yaliyokuwa yanakaribia kuvunwa katika mashamba yenye jumla ya hekta 90.5 Kata ya Chita, Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.
Akizungumza na HabariLeo, Bwana Shamba wa Kata hiyo, Philbert Lawrent, amesema tatizo la panya hao limekuwa kubwa katika vijiji viwili vya Chita na Makutano, kati ya vitano vilivyopo.
Amesema wamekuwa wakifanya jitihada za kuwadhibiti panya hao kwa kutumia njia za kienyeji pamoja na sumu.
Ametaja njia hizo kuwa ni kuchimbia ndoo chini na kuweka maji kisha kuzungushia pumba pamoja na kupurua miti ya mahindi, ili panya hao washindwe kupanda.
Amesema kwa kuwa tatizo ni kubwa wakulima hao wanaweza wasiambulie hata kidogo mazao waliyoyapanda.
Mkulima Hedrick Magome aliyelima alizeti na mahindi katika Kata ya Chita, amesema amelima eka sita mahindi ambayo yamefikia hatua ya kuchomwa na alizeti hatua ya kuchanua, kisha wakazuka panya kwa wingi walioanza kula mazao hayo.
” Kwa kipindi cha wiki moja wameshambulia mahindi nimeambulia kuvuna machache, ambayo ni mabichi ambayo nimewapa nguruwe, nasi tumetumia na majirani,” amesema.
Kwa maelezo yake walipoanza kula alizeti alinunua sumu lakini haikusaidia kutokana na wingi wa panya hao.
” Nilishauriwa ninunue ndoo za lita 20 nichimbie chini na kuweka maji nusu kisha nizungushie pumba, ikiwa ni njia ya kuwatega panya hao, nilinunua majaba na kuchimbia, Siku ya kwanza nilitoa panya 200, kila siku waliongeza hadi kufikia 1000 kwa siku,” amesema.
Ameongeza kuwa hivi sasa hata kuwatoa anaona kinyaa wamenaswa wengi, hivyo ameamua kuwaacha.
Amesema panya hao walianza mashambulizi mwishoni mwa Agosti mwaka huu, amejitahidi kuwadhibiti bila mafanikio.