KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amemteua Askofu Mkuu Protase Rugambwa kuwa Askofu Mkuu Mrithi wa Jimbo Kuu la Tabora.
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk Charles Kitima ameeleza hayo alipozungumza na HabariLEO jana.
Dk Kitima alisema uteuzi huo wa Papa umefanyika baada ya Askofu wa jimbo hilo, Paul Ruzoka muda wake wa kustaafu kukaribia.
“Askofu Mkuu Ruzoka anatarajia kustaafu ndani ya mwaka huu kwa hiyo Askofu Mkuu Rugambwa anaenda pale kujiandaa kurithi, siku Askofu Ruzoka akistaafu tu huyu anarithi,” alisema Dk Kitima.
Alisema Askofu Mkuu Ruzoka anatarajia kustaafu atakapofikisha umri wa miaka 75 ndani ya mwaka huu akiwa Askofu Mkuu wa tatu wa jimbo hilo.
Maaskofu waliomtangulia Ruzoka ni Askofu Mkuu Marko Mihayo aliyeongoza kuanzia mwaka 1960 mpaka 1985, Askofu Mkuu Mario Mgulunde (1985-2006) na Askofu Mkuu Rugambwa atakuwa Askofu Mkuu wa nne.
Dk Kitima alisema Jimbo Kuu la Tabora ni jimbo la pili kuanzishwa nchini mwaka 1878 likitanguliwa na Jimbo Kuu la Dar es Salaam ambalo lilikuwa la Bagamoyo mwaka 1868.
Alisema kuanzia mwaka 1878 hadi mwaka 1953, Tabora lilikuwa jimbo la kawaida na kuanzia mwaka huo lilipandishwa hadhi na kuwa Jimbo Kuu.
Baada ya uteuzi huo, alisema Askofu Mkuu Rugambwa anatarajiwa kuwasili jimboni katika kipindi cha miezi miwili baada ya likizo yake kukamilika kwa kuwa kwa kawaida askofu anapoteuliwa anakuwa na haki ya likizo.
Dk Kitima alisema Askofu Mkuu Rugambwa aliwahi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2012 alipohamishiwa Vatican.
Pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Congregasio ya Uinjilishaji Vatican.