‘PDPC itasaidia kulinda faragha, taarifa binafsi’

DAR ES SALAAM: Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuzinduliwa kwa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) kutasaidia kulinda faragha ya mtu binafsi na familia yake kwa ujumla.

Pia amesema kuna umuhimu wa faragha katika taarifa binafsi, ndiyo maana serikali imeamua kutunga sheria na kuwa na tume hiyo.

Rais Samia ameyasema hayo leo Aprili 3, 2024 katika uzinduzi wa tume hiyo uliofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam na kusema kuwa kila mwanadamu ana utashi na staha, hivyo zipo baadhi ya taarifa asingependa zitolewe na kujulikana kwa kila mtu.

“Na kwa ukweli ingekuwa taarifa zetu zote ziko wazi na watu wanazijua tusingetazamana usoni, au dunia ingekuwa ya aina nyingine hakuna faragha, hakuna staha,”amesema.

Amesema, zipo baadhi ya taarifa ambazo zinaweza kutumika kuhujumu jamii nzima na wakati mwingine kusababisha unyanyapaa kwa watu wengine mfano daktari aliyekosa uadilifu akitoa taarifa za ugonjwa wa mtu au wa kurithi unaweza kusababisha familia au mtu kunyanyapaliwa.

“Unaweza kutoa taarifa ya mtu na ikaleta vurugu kwenye jamii, vita na hata mauaji,”amesema.

Amesema kuna kila haja ya kuwa na sheria hiyo kwa kuzingatia maendeleo makubwa ya kiteknolojia taarifa binafsi za watu zinaweza kukusanywa, kuchakatwa na kutumika bila ya wahusika kufahamu.

“Ni mara ngapi tunasikia taarifa zinatoka, hii sio sawa, licha ya taarifa binafsi kutumika kwa hujuma lakini pia taarifa binafsi ni biashara kubwa kwa makampuni mbalimbali ya kimtandao, hivyo hatuna budi kulindana,”amesisitiza Rais Samia.

Habari Zifananazo

Back to top button