Pialali, Mfaume mwisho wa ubishi

PAMBANO linalosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa masumbwi nchini, kati ya bondia Idd Pialali na Mfaume Mfaume linatarajiwa kufanyika leo kwenye kwenye ukumbi wa kimataifa wa mikutano mkoani Arusha (AICC).

Pambano hilo lisilokuwa la ubingwa la raundi 12 litakuwa la kwanza kuwakutanisha mabondia hao wawili ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitupiana vijembe kwenye vyombo vya habari.

Katika rekodi zao tangu walipoingia katika ngumi za kulipwa Mfaume mwenye nyota moja na nusu amecheza mapambano 27 huku kati ya hayo ameshinda mara 17, sare mbili na kupoteza mara nane.

Pialali mwenye nyota mbili rekodi zake katika ngumi za kulipwa zinaonesha amecheza michezo 39 kati ya hiyo ameshinda mara 30 huku akipoteza mapambano nane na sare moja.

Akizungumza na gazeti hili juzi, Mfaume alisema kuwa ni wakati wa kuweka heshima yake kwa mabondia wa ndani na Pialali, atakuwa mfano kwao kwa kile atakachoenda kukutana nacho ulingoni.

“Nimekuwa nikipokea kejeli na maneno maneno sasa ni wakati wa vitendo nataka kuwaonesha kuwa huwa sibahatishi kwenye kazi zangu najua kiu ya mashabiki wangu ni kuona naibuka na ushindi katika pambano kesho (leo),” alisema Mfaume.

Naye Pialali, alisema kuwa huu ndio wakati wa yeye kuonesha kuwa ndio mfalme wa Dar es Salaam, atalitumia pambano hilo kuthibitisha ni kwanini amefikia nyota mbili kwenye mchezo wa ngumi za kulipwa.

“Amekuwa ananikimbiakimbia mara kadhaa nashukuru ameingia kwenye mikono yangu nataka nimuoneshe kwanini niko juu yake kwenye viwango vya ubora ila namuonya asije akaingia na akili kuwa ataniponyoka hilo asahau na sitomruhusu amalize raundi zote,” alisema Pialali.

Mapambano mengine yatakayochezwa leo Karim Mandonga atapanda ulingoni dhidi ya Ali Baba, Halima Vunjabei atamkabili Zawadi Kutaka naye Shaban Ndaro ataoneshana umwamba na Shaban Kaoneka.

Wengine ni Batuli Yassin atakayemkabili Loveless Kokha naye Said Faraji atavaana na Osama Arabi, Hassan Ndonga dhidi ya Ramadhan Kumbele, na Yohana Mchanja atamkabili Haidary Mchanjo.

Habari Zifananazo

Back to top button