PIC: Stamico ifanye uwekezaji wenye tija

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imelitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kubana matumizi na kufanya uwekezaji wenye tija ili waweze kutoa gawio kwa serikali.

Rai hiyo ilitolewa juzi na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Vuma Agustino wakati wa ziara ya siku moja katika mradi wa kiwanda cha Mwanza Precious Metals Refinery (MPMR).

“Mradi huu ni mzuri sana na unamilikiwa na Stamico. Mradi huu unatakiwa kuleta tija katika jamii na mradi huu ni mradi wa kisasa na una thamani zaidi ya Sh bilioni 16,” alisema Agustino.

Advertisement

Aliipongeza Wizara ya Madini kwa kufanya vizuri katika kuisimamia Stamico kufanya uwekezaji huo. “Shirika la Stamico mwaka 2017 lilikuwa shirika lililokuwa likitengeneza hasara kubwa sana mpaka ilifika hatua kamati tulitaka kushauri serikali ilifute kabisa,” alisema Agustino.

Aliahidi kamati yao itaendelea kusimamia serikali na mashirika yake ili yaweze kufanya uwekezaji wenye tija. Mwenyekiti wa Bodi ya Stamico, Meja Jenerali Micheal Isamuhyo aliahidi shirika lao litafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na kamati ya bunge.

“Ziara kama hizi za viongozi zinatusaidia katika kuongeza ufanisi wa kiwanda hiki na kitakuwa na manufaa makubwa sana,” alisema Isamuhyo. Waziri wa Madini, Dotto Biteko alisema serikali imeamua madini yote yanayosafirishwa yawe yanasafishwa kwanza kabla ya kusafirishwa.