PIC yabaini matumizi makubwa ulipaji gharama huduma NHIF

KAMATI ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) imebaini  matumizi makubwa ya kulipa gharama za huduma za wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) hali inayotishia uhai wa mfuko.

Pia imetaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuandaa mpango kazi ndani ya siku 30 wa namna walivyojipanga kukabiliana na hoja za kikaguzi zilizobainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Hayo yamebainishwa Alhamis na  Mwenyekiti, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma, Jerry Silaa baada ya kukutana na kujadiliana na NHIF kuhusu taarifa za uwekezaji na hesabu za Mfuko huo kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

Alisema kutokana na hali hiyo, kamati imeishauri NHIF kuja na mkakati maalumu wa kuongeza wanachama zaidi.

“Baada ya kujadiliana tumekuja na maelekezo matatu ikiwamo ya kutaka mfuko kuja na mpango wa kuongeza idadi ya wanachama kwa sababu hesabu za NHIF zimeonesha matumizi ni makubwa kwa maana ya malipo ya huduma za wanachama yanaongezeka ukilinganisha na mapato wanayokusanya, na hii inahatarisha uhai wa mfuko,” alisema.

Silaa alisema pia kamati imeuagiza mfuko kuwa na jitihada za makusudi za kuwa na utaratibu mzuri wa kudhibiti matumizi.

Alisema wameutaka kuhakikisha wanaimarisha mifumo ya Tehama kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na udhibiti wa mianya ya vitendo vya udanganyifu.

Katika hatua nyingine, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeitaka TRA kuandaa mpango kazi ndani ya siku 30 wa namna walivyojipanga kukabiliana na hoja za kikaguzi zilizobainishwa na CAG.

Makamu Mwenyekiti wa PAC, Japhet Hasunga alisema mpango huo unapaswa kuwasilishwa kwenye kamati hiyo ili kuona utekelezaji wake.

“Tumeagiza mifumo yote ya ukusanyaji wa mapato ya serikali ionane ifikapo Juni 30, mwaka 2023,” alisema.

Alibainisha kuwa hoja zinazotakiwa kutengenezewa mpango kazi zinatokana na mifumo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya forodha.

“Unakuta mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani hauonani na mfumo wa makusanyo wa forodha au mingine, ikiwa haionani huwezi kuwa na taarifa timilifu,” alisema.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button