PIC yaipongeza serikali uwekezaji mashirika ya umma

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) imeipongeza serikali kwa kuwekeza zaidi ya Sh trilioni 70 kwenye mashirika ya umma.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jerry Silaa ametoa pongezi hizo jijini Mwanza wakati akizungumza baada ya kamati hiyo kuitembelea Bandari ya Mwanza kuona utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa meli ya Mv Mwanza Hapa Kazi Tu.

Silaa alisema hakuna mradi wowote wa kimkakati au wa maendeleo uliotengewa fedha na umesimama na wakati wa ziara kwenye mikoa mbalimbali wamekuta kazi za miradi zinaendelea.

Alisema ujenzi wa meli ya Mv Mwanza Hapa Kazi Tu, reli ya kisasa (SGR) hadi mkoani Mwanza na daraja la JPM vitaufungua mkoa huo kiuchumi.

“Mkoa wa Mwanza utarudi kwenye sura yake ya kuwa ‘hub’ kwenye maeneo nchi jirani za Uganda, Rwanda na Burundi ambayo mizigo yake inaweza kupitia hapa,” alisema Silaa.

Alisema PIC kwa mujibu wa Ibara ya 62 (ii) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni kuishauri na kuisimamia serikali na kupitia mradi huo wa meli ya Mv Mwanza Hapa Kazi Tu Kamati imeona ni jinsi gani serikali inafanya kazi yake na kwa kutimiza wajibu wake.

“Tumeridhika na kazi zinazofanyika hapa Mwanza, naamini uwekezaji wa mitaji ya umma unafanyika vizuri,” alisema. Mtendaji Mkuu wa MSCL, Eric Hamissi alisema meli ya Mv Mwanza Hapa Kazi Tu inatarajiwa kukabidhiwa serikalini katika kipindi cha miezi sita ijayo.

Hamissi alisema dhamira ya serikali meli itakapokamilika itakuwa imetumia gharama ya dola za Kimarekani milioni 46.9 sawa na Sh bilioni 109.15. “Hatua ambayo imefikia nzuri kuelekea ukamilishaji wake,” alisema na kuongeza kuwa meli itakapokamilika itakuwa na uzito wa tani 3,500.

Habari Zifananazo

Back to top button