PIC yaridhishwa na usimamizi wa miradi

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi inazofanya za ujenzi wa miradi mya kimkakati.

Mwenyekiti wa Kamati ya PIC, Jerry Silaa alitoa pongezo hizo wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Mwanza, Wilaya ya Misungwi na Menejimenti ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wakati kamati hiyo ilipotembelea mradi huo.

“Kote tulikopita kwenye ziara yetu hii, miradi ya umeme, maji, barabara na madaraja yote inaendelea, hakuna kazi iliyosimama,” alisema Silaa.

Alisema serikali inatekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya ‘kazi iendelee’ na akasema kamati hiyo imekasimiwa madaraka ya Bunge kwenye eneo la uwekezaji na kwamba hakuna kazi ama mradi wowote uliosimama.

“Nchi kwa sasa inafunguka kiuwekezaji kwa sababu watu wenye mazao yao na biashara zao, wanaotaka kwenda nchi jirani, utalii wote watavuka kwa uhakika kupitia daraja hili,” alisema Silaa.

Aliiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi isimamie mradi wa ujenzi wa daraja la JPM linalojengwa katika eneo la KigongoBusisi ukamilike ifikapo Februari 24 mwakani.

“Daraja hili ni la kimkakati linalounganisha ushoroba wa ziwa Victoria kutoka mpaka wa Sirari mpaka Mtukula na ule wa Rusumo – Uganda ili liweze kuwa na tija iliyokusudiwa,” alisema Silaa.

Aliutaka pia uongozi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi uweke mpango utakaowezesha miradi mikubwa iliyo chini ya Tanroads iwe na miradi ya ziada ya huduma ya jamii.

“Hatua hii itasaidia kuongeza hamasa kwa wananchi kwa kuwa watakuwa wamepata manufaa yanayotokana na mradi na hivyo kuweza kupata ushirikiano kwenye miradi hiyo inayotekelezwa na wakala,” alisema Silaa.

Aliuagiza uongozi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi uandae kipindi kuhusu ujenzi wa daraja hilo la kihistoria na litangazwe kwenye vyombo vya habari vya kielektroniki na magazeti ili Watanzania waweze kuona kazi ya kihistoria inayoendelea kufanywa kupitia kwenye mradi huo.

“Naamini kupitia Tanroads wanaovuka na malori katika eneo hili na wananchi wahojiwe maana kazi hizi lazima zitangazwe ili watu wafahamu kuwa kazi inaendelea,” alisema Silaa na kuongeza: “Ni lazima mumuoneshe mtu kwamba asilimia hizi zimekamilika kwenye mradi na kazi gani zimekwishafanyika na documentary hiyo itawasaidia sana Watanzania wote kufahamu ujenzi wa mradi huu”, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Rogatus Mativila alisema ujenzi wa daraja hilo la JPM unaogharimu Sh bilioni 716.333 hadi Machi 8 mwaka huu umefikia asilimia 70.

Habari Zifananazo

Back to top button