PIGO kwa Nigeria ambapo mshambuliaji, Victor Boniface anayekipiga Bayer Leverkusen atakosa AFCON huku ikielezwa kuwa huenda akawa nje kwa miezi miwili kutokana na jeraha la misuli.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 ndiye mchezaji wa kwanza kupata jeraha kwa walioitwa hivi karibuni kabla ya michuano hiyo itakayoanza Januari 13 mjini Abidjan.
Mshambulizi wa Nice Terem Moffi ameitwa kuchukua nafasi ya Boniface, huku akisubiri idhini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) na makubaliano na klabu ya mchezaji huyo inayoshiriki Ligi ya Ufaransa ya Ligue 1.
Boniface sasa anajiunga na orodha ya wachezaji wa Nigeria ambao wamelazimika kukosa Afcon 2023 kutokana na majeraha, akiwemo mshambuliaji wa Nottingham Forest Taiwo Awoniyi na kiungo wa Leicester City Wilfred Ndidi.