SERIKALI imewataka maofisa ugani wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha kuzitumia pikipiki zilizowakabidhi kuleta tija ya kilimo bora na ufugaji wa kisasa kwa wananchi na sio kuzitumia kama kitega uchumi kwa kujitafutia kipato.
Akizungumza wakati wa kukabidhi pikipiki saba kwa maofisa ugani, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Emmanuela Kaganda amesema hategemei kusikia pikipiki imeibiwa ama ikitumika kama bodaboda mitaani.
“Yeyote atakaye tuletea habari za kuibiwa kwa pikipiki hizi hivi karibuni kweli tutamchukulia hatua Kali.”Amesema DC Kaganda
Sambamba na hilo Kaganda ameagiza pikipiki hizo zikatumike kwa makusudi yaliyokusudiwa kwa ajili ya kuwafikia wafugaji na wakulima katika eneo la Halmashauri hiyo Ili wananchi hao wakanufaike na matunda ya Serikali yao
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya ya Arusha Suleiman Msumi amesema wakazi wa halmashauri hiyo wengi wao ni wakulima na wafugaji hivyo kwa uwepo wa pikipiki hizo zinakwenda kuwa mkombozi na kabadilisha maisha ya wananchi wa halmashauri hiyo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Arumeru, Noel Severe amesema pikipiki hizo zitatatua kero ya maofisa ugani kutokufika kwa wananchi kwani hapo awali amekuwa akipokea kero kwa wananchi juu ya maofisa ogani hao kutokufika kwa wananchi.
Maofisa ugani wameishukuru Serikali na wameeleza pikipiki hizo zitawaongezea ufanisi katika kutekeleza majukumu yao kwani kutokana na ukubwa wa maeneo ya kazi ilikuwa inawapa ugumu kufikia wananchi wote.