Pinda ahimiza busara utatuzi migogoro ya ardhi

MWANZA: NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda amewataka watumishi wa sekta ya ardhi nchini kutumia busara wakati wote wa kushughulikia changamoto za sekta ya ardhi.
 
Pinda ametoa kauli hiyo leo tarehe 11 Machi 2024 wakati wa uzinduzi wa Kliniki ya Ardhi katika mkoa wa Mwanza ilinayofanyika viwanja vya Nyamagana
 
‘’Busara itutangulie wakati tunaenda kutatua migogoro ya ardhi tusimuangalia mtu kwa hali yake bali tumuangalie kwa haki yake,’’ amesema Pinda.
 
Amesema, watendaji wa sekta ya ardhi wasiposimamia katika kuwatafutia haki wananchi watasababisha malalamiko yasiyo na tija lakini pia hawataifariji nchi na badala yake watatengeneza malalamiko.
 
Amewaambia watumishi kuwa, kwa namna Wizara ya Ardhi inavyofanya mabadiliko yakiwemo yale ya kimfumo hakutakuwa na nafasi kwa mtu atakayeharibu eneo moja kuhamishiwa eneo lingine.
 
Amewaasa watendaji wa ardhi kufuata sheria na kuwa na maadili mema wakati wote wa kutekeleza majukumu yao pamoja na kujiepusha kabisa vitendo vya rushwa. ‘’Zingatieni mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa kuwa Wizara yetu ndiko inakoelekea.

Pia mdumishe amani, upendo na ushirikiano wakati wa kutekeleza majukumu yenu

 
Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi ameitaka Ofisi ya Aradhi mkoa wa Mwanza kuhakikisha inaharakisha utoaji hati milki za ardhi na kuongeza kuwa wizara yake haitasita kumchukulia hatua mtumishi yeyote atakayekwamisha kazi hiyo.
 
Kwa mujibu wa Pinda, Wizara ya Ardhi inakamilisha maboresho ya mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) utakaoruhusu huduma na miamala ya sekta ya ardhi kutolewa kidigitali. Mfumo huo utaanza kutumika hivi karibuni kwa kuanza na mikoa ya Arusha, Tanga, Mwanza na Mbeya.

Habari Zifananazo

Back to top button