Pinda ahimiza umwagiliaji kumaliza umaskini nchini

WAZIRI Mkuu mstaafu na Mwenyekiti wa Baraza la Rais la Chakula na Kilimo, Mizengo Pinda ametaka msukumo zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji ili kumaliza umaskini hasa maeneo ya vijijini.

Pinda alisema hayo Dodoma jana wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Shirika linalojishughulisha na ukuaji endelevu wa mifumo ya chakula Afrika (AGRA). Mpango huo utagharimu Dola za Marekani milioni 60.

Mpango mkakati huo wenye kaulimbiu ya ‘Kuchochea masoko jumuishi na yenye ushindani katika kilimo ili kuleta mabadiliko kwenye mifumo ya chakula nchini’, umezinduliwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.

Pinda alisema pamoja na kutambua mafanikio ambayo Tanzania imefikia, bado kuna kazi ya kukabili umaskini mkubwa uliopo vijijini na akasema kilimo cha umwagiliaji ni moja ya njia ya kusaidia kuongeza uzalishaji na kuinua vipato vya wananchi. “Tuna ardhi, tuna kila kitu kinachohitajika.

Tunachohitaji kufanya ni kuweka kipaumbele katika maendeleo na uboreshaji wa mifumo ya chakula ili kujenga maisha endelevu na kuinua jamii za vijijini,” alisema Pinda. Aliongeza: “Tumefanya vizuri katika maeneo mengi na kubwa ni utulivu wa nchi yetu…mfumo wetu wa chakula haujapewa nafasi ya kutosha… kufungua uelewa zaidi juu ya hali ya nchi na umuhimu wa kuongeza kasi ya kutumia ardhi yetu ipasavyo na ndani ya kipindi kifupi.”

Pia alisema kuna umuhimu wa nidhamu ya kazi na kujikita katika teknolojia za kisasa kama walivyo Israel ambao hawana mito lakini wana kilimo cha umwagiliaji chenye tija. “Israeli ina maji gani kuishinda Tanzania? Wanatumia maji ya bahari wameyabadilisha na kuwa maji yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, mashamba yao yana mifumo ya umwagiliaji,” alisema Pinda na kuipongeza AGRA kwa kuja na mkakati huo.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akiwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli alisema serikali imeweka kipaumbele katika sekta ya kilimo ili kutengeneza maisha zaidi huku ikihakikisha vijana na wanawake wanajumuishwa.

“Tanzania inalenga kuwa ghala la chakula kwa Afrika na dunia nzima. Tumejitolea kufungua uwezo wa sekta ya kilimo, ambayo kwa sasa inachangia asilimia 25 ya Pato la Taifa na ni chanzo kikuu cha fedha za kigeni na chanzo cha ajira na utajiri,” alisema Bashe.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema serikali itatoa ushirikiano wa kutosha wakati wa kutekeleza mpango huo. Mkuu wa Kikanda wa AGRA Afrika Mashariki, Profesa Jean Jacques Muhinda alisema taasisi hiyo katika miaka hiyo mitano imelenga kuunga mkono juhudi za Tanzania kuwa na uzalishaji mkubwa wa chakula.

Habari Zifananazo

Back to top button