Pinda apendekeza adhabu ya kifo ifutwe

WAZIRI Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amependekeza adhabu ya kunyongwa hadi kufa inayotolewa na mahakama kwa makosa ya kuua kwa kukusudia na uhaini, iondolewe na badala yake iwe kifungo cha maisha jela.

Pinda amesema adhabu hiyo haina tija kuwafanya watu wasifanye makosa hayo, bali kinyume chake wakiwa na utaratibu mwingine wa kuwapatia matumaini, wanaweza kubadilisha tabia.

Alisema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasilisha mapendekezo kwa Tume ya Kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za Haki Jinai nchini.

Pinda alisema adhabu ya kunyongwa haimpi fursa aliyehukumiwa kubadilisha tabia na kurudi katika jamii hivyo mahakama itoe adhabu ya kifungo cha maisha jela.

Alisema katika kipindi hicho, aliyetiwa hatiani aendelee kufanyiwa marekebisho ya kisaikolojia.

“Hii principal ‘kanuni’ ya kuua na kisha kuuawa hapana, labda ka-Ukristo kangu kananifanya nione si sawa, lakini nchi nyingi zilishaondoa vitu hivi, hivyo nasi tuone namna ya kubadilisha adhabu na iwe ya kifungo cha maisha jela,” alisema Pinda.

Aliongeza: “Hili jambo nimeona nakereketwa nalo, kwangu adhabu ya kunyongwa mtu inanipa tabu kwa sababu ni kweli alitoa roho ya mtu katika mazingira yake, lakini ili kumkomesha tumnyonge hili ni kosa juu ya kosa na sidhani kama inatibu ugonjwa huu.”

Adhabu ya kifo inatolewa chini ya Kifungu cha 197 cha Kanuni za Adhabu Sura 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Licha ya wadau kupendekeza adhabu hiyo kuondolewa kwa kile walichodai inavunja haki za binadamu, imekuwa ikiendelea kutolewa kwa kuwa sheria haijabadilishwa.

Kuhusu magereza, Pinda alisema magereza wanapaswa kuwafuatilia wafungwa wote wanaopitia urekebishaji na kuachiwa kwa sababu ya kujirekebisha tabia ili kujua wako wapi na wanafanya nini.

Alieleza jukumu hilo linaweza kufanywa na magereza au ofisi ya ustawi wa jamii ili kupata matokeo kama urekebishaji huo umefanikiwa.

Pia alisema jeshi hilo linapaswa kuwatoa watoto wanaozaliwa kwenye magereza kwani kuwaacha huko, huwaathiri kisaikolojia hivyo watolewe na kuunganishwa na taasisi nyingine ambazo zitawalea.

“Hii itakuwa rahisi kwa mama huyu akitoka magereza ataambiwa mtoto wake yupo wapi kuliko kukaa gerezani ambako mazingira yake sio rafiki na aina ya vyakula wanavyokula haviwastahili mama na mtoto wake,” alisema Pinda aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kuanzia Februari 9, 2008 hadi Novemba 5, 2015.

Akizungumzia tume hiyo, alisema vyombo vinavyoguswa moja kwa moja na haki jinai ni Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Mahakama na Magereza.

Alisema kuna malalamiko mengi ya wananchi katika mifumo ya haki jinai na ndio maana Rais Samia Suluhu Hassan aliunda tume hiyo.

“Kazi iliyopo mbele ya tume hii ni kuona namna haki inasimamiwa katika Maeneo ya makosa ya jinai. Mtuhumiwa ahudumiwe kulingana vipi kwa kuzingatia haki zake mpaka jambo lake liishe, nawahurumia kwa sababu kazi hii sio ndogo,” alisisitiza.

Alishauri pamoja na kuainisha makundi mbalimbali kupata maoni yao, waone maeneo ya malalamiko na kukutana na wadau ili wawasikilize ili kupata uhalisia wa masuala yanayolalamikiwa.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Frederick Werema amesema adhabu ya kifo si adhabu kwa sababu haimpi nafasi mshitakiwa kurekebisha tabia yake, lakini ibaki katika sheria ili iwe tishio.

“Adhabu ya kifo ibaki kwenye sheria kama tishio kwa watu kutotenda makosa hayo, lakini kuna watu wanafanya mauaji ya kinyama ambao wanastahili kunyongwa hadi kufa,” alisema Jaji Werema.

Alisema kuna wakati adhabu hizo ni ngumu kuzitoa, lakini wanafungwa mikono na sheria na hivyo kuamuru adhabu ya kifo.

Jaji Werema amesema majaji na mahakimu wanapaswa kutumia mamlaka yao kufuta kesi ambazo hazina ushahidi ili kupunguza mlundikano.

Habari Zifananazo

Back to top button