MAMLAKA ya Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) imepiga marufuku bidhaa aina ya Lump Sugar maarufu ‘Vipipi utamu’ vinavyodaiwa kutumiwa na baadhi ya wanawake kwa ajili ya kuongeza hamu ya tendo la ndoa.
Taarifa ya ZFDA imetoa tahadhari ya kutotumika kwa pipi hizo kwa kile kilichoelezwa kuwa na madhara, huku ikiendesha msako mkali wa kuzikamata bidhaa hizo ili kuziondoa sokoni.
Hatua hiyo ya ZFDA imekuja kukiwa kuna matangazo ya bidhaa hizo za Pipi utamu kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, ikizinadi huku wanawake wakiwa ndio wateja wakuu, zikielezwa kuwa na uwezo wa matumizi mbalimbali yahusiyo tendo la ndoa.
Pipi hizo huuzwa kati ya Sh 5,000 hadi Sh 10,000, ambapo ZFDA imesema imemkamata mmoja wa wafanyabiashara wa pipi hizo, Mariam Shaban Laurent na kumzuia kuendelea kufanya biashara ya pipi hizo zinazodaiwa pia kusaidia kubana maumbile ya watumiaji.
Mkuu wa Divisheni na Vipodozi wa ZFDA, Salum Hamad Kassim, amesema wamechukua sampuli za pipi hizo na kuzipeleka kwa Maabara Kuu ili kujiridhisha.
Amesema bidhaa hizo ni hatari kwa kuwa hazina lebo, hazina ujazo wala muda wa kuisha matumizi na vile vile haijulikani zinatoka wapi.
Kwa upande wa mfanyabiashara huyo, Mariam Shaban Laurent amesema amekua akifanya biashara yake hiyo kwa njia ya mtandao.
“Wateja wote huwa nawahakikishia bidhaa haina madhara na ni asili, sitofanya tena biashara hii hadi hapo Mamlaka itakapotoa ripoti, ” amesema.
Kauli ya daktari
HabariLeo imezungumza na daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Fabian Tumai kuhusu matumizi ya pipi hizo kiafya, ambapo amesema ni hatari kwa watumiaji kwani wanajiweka kwenye hatari kwa kutumia vitu visivyofaa na kujisababishia magonjwa, ikiwamo saratani.
Dk Fabian anasema hakuna dawa ambayo imethibitishwa kuwa ina uwezo wa kumuongezea mwanamke hamu au nguvu ya kushiriki tendo la ndoa, kinachofanywa na wafanyabishara hao ni kutafuta fedha.