Polisi fuateni dhima ya jeshi
RAIS Samia Suluhu Hassan Jumatano alikutana na kuzungumza na viongozi wa Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro ambako pamoja na mambo mengine alisisitiza jeshi hilo suala zima la nidhamu na uadilifu kwa askari wake.
Kama sehemu ya kuonesha uwepo wa tatizo hilo la nidhamu ndani ya Polisi, Mkuu wa Jeshi hilo nchini, IJP Camilius Wambura, amesema jeshi hilo katika kipindi cha Januari hadi Julai mwaka huu limewafuta kazi askari wake 45 kati ya 265 walioshitakiwa kutokana na makosa mengine ya jinai.
Napongeza Jeshi la Polisi kwa hatua hiyo kwa kuwa ndio misingi ya kuanzishwa kwa chombo hicho ndani ya taifa hili ambalo tangu lilipopata uhuru wake limekuwa likisifiwa na mataifa mengine kwa uadilifu wa viongozi wake na wananchi kwa ujumla.
Mbali na pongezi kwa jeshi hilo, kwa dhati kabisa napenda kutoa pongezi zangu kwa IJP Wambura kwa kuanza kuchukua hatua mbalimbali kwa askari wake wanaoonekana kwenda kinyume.
Naamini madhumuni ya uwapo wa askari polisi pamoja na viongozi wake ndani ya taifa hili umelenga kulinda usalama wa raia pamoja na mali zao hivyo niwatake viongozi wakuu wa jeshi hilo kutochoka kuendelea kuwaadhibu askari wake wote wanaokwenda tofauti.
Hatua hiyo itarejesha heshima ya jeshi na kulinda misingi ya jeshi hilo na kuwa fundisho kwa walinzi wanaotakiwa kuwa mfano na kujiingiza katika kudhalilisha jeshi.
Yapo mambo mengi ameyataja ndani ya Jeshi la Polisi kama changamoto katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali iliyopewa ambayo yanaweza kutatuliwa.
Mathalani, hivi karibuni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Abdulrahman Kinana aligusia baadhi ya kero zinazosababishwa na baadhi ya askari wa usalama barabarani na kwa ushauri wake akaomba wapunguzwe badala ya uwapo wa idadi yao kubwa barabarani usio na tija.
Kwangu mimi tatizo halikuwa idadi kubwa ya uwapo wao barabarani bali nini wanakifanya katika maeneo hayo ya kazi wakati wanapotekeleza jukumu hilo la usalama wa maisha ya watu pamoja na vyombo vyao maana wengi tunajua, tumelia na kulalamika.
Ninachoamini kama ndugu zetu polisi watasimamia misingi ya mafunzo yao waliyopewa chuoni na kuyafanyia kazi ni wazi kuwa jeshi letu hilo lingekuwa moja ya majeshi yenye ufanisi mkubwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati na kujizolea sifa kedekede.
Pamoja na hayo nisiwe mchoyo wa fadhila kwa kuwapa kongole askari wote wanaosimamia misingi ya utumishi wa jeshi hilo nikiwaombea waendelee kubaki hivyo na hata kuvirithisha vizazi vyao tabia njema.