‘Polisi isibague wafupi katika ajira’

Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohamed Ali 'Kawaida'.

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umemwomba Rais Samia Suluhu Hassan Jeshi la Polisi lisiwabague watu wafupi katika nafasi za kazi na mafunzo wanayoyatoa.

Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohamed Ali Mohammed maarufu Kawaida, amelaumu jeshi hilo kukataa vijana wafupi na kuwapa kipaumbele warefu.

Kawaida alisema hayo Paje Zanzibar wakati Rais Samia akihitimisha matembezi ya UVCCM kuadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoshirikisha vijana 500 wa mikoa yote nchini.

Advertisement

Alisema usalama wa raia na mali zao ni jukumu la kila kijana na hauchagui rangi, kimo wala umbile hivyo Polisi wanapotangaza nafasi za mafunzo na ajira wasiwabague wafupi.

“Hivi karibuni Jeshi la Polisi limetangaza nafasi za ajira lakini katika mambo ambayo vijana wameniomba niliseme ni kuhusu sisi wafupi, wanatukataa na kuwapa kipaumbele wale wenzetu warefu lakini wanasahau kwamba jukumu la ulinzi na uslama ni la kwetu sote,” alisema Kawaida.

Katibu Mkuu wa UVCCM, Kenan Kihongosi alisema wanaenzi, kuheshimu na kulinda kwa vitendo mapinduzi hayo na kwamba wataendeleza na kuishi historia ya wazee wao waliofanya mapinduzi kuangusha utawala wa kisultani na Wazanzibari kujitawala.

Kihongosi alisema matembezi hayo yalihusisha ukaguzi na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa kukagua viwanja vya michezo, makazi ya wazee, usafi wa mazingira na mradi wa tangi la maji.