Polisi Shinyanga yanasa noti bandia
JESHI la polisi mkoani Shinyanga limefanikiwa kukamata noti bandia 15 za Sh 10,000 jumla zikiwa 150,000 pamoja na silaha aina ya Shortgun Belgium yenye namba 18342 ambayo ilikuwa inamilikiwa kinyume na sheria.
Pia wamekamata silaha Shortgun Pump Action yenye namba za usajili Tz CAR 69657A ambayo ilitumika katika tukio la unyang’anyi na kutelekeza baada ya kugundua kuwa wanafuatiliwa na askari.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Janeth Magomi alisema hayo jana mbele ya waandishi wa habari ambapo alieleza katika msako na doria kwenye maeneo mbalimbali katika mwezi Agosti na Septemba.
Kamanda Magomi alisema katika msako huo walifanikiwa kuwakamata waganga wa kienyeji watatu waliokuwa wakifanya shughuli za uganga bila kuwa na kibali huku wakitumia vifaa mbalimbali vya ramli chonganishi.
Kamanda Magomi alisema wamekamata mashine moja ya kufua umeme,mashine ya kuchomelea vyuma na lita 120 za mafuta ya kuendeshea mitambo pamoja na nondo 880.
“Jumla ya watuhumiwa 12 wanashikiliwa kuhusiana na makosa hayo na wengine wamefikishwa kwa hatua za kisheria huku wengine wakipewa dhamana wakisubiri upelelezi”alisema Kamanda Magomi.
Kamanda Magomi alisema wamekata dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilogramu 40 na kete18, heroin kete moja na pikipiki 16 zilizokuwa zikitumika katika kuendeleza makosa ya kiuhalifu.
“Jumla ya pikipiki 786 zilikamatwa kwa makosa mbalimbali ikiwa pikipiki mbovu zilikuwa 59,kutovaa kofia ngumu madereva 182 na kuzidisha abiria madereva 76”alisema kamanda Magomi.
Kamanda Magomi alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi kufichua wahalifu kwa kutoa taarifa na kuwataka wanaoviendeleza kuviacha.