Polisi: Silaha hairithiwi

PWANI; Kibaha. Usalimishaji silaha za moto kwa hiari unaofanyika nchi nzima umeonesha mafanikio makubwa, ambapo silaha zilizosalimishwa zimeongezezeka kutoka silaha 228 mwaka 2021 hadi kufikia silaha 1,220 mwaka 2022.

Kutokana na hali hiyo Jeshi la Polisi limesisitiza wananchi ambao wanamiliki silaha kinyume cha sheria wazisalimishe silaha zao, wakiwemo wale ambao wamekaa na silaha ambazo wamiliki wake halali wamefariki dunia.

Akizungumza mkoani Pwani wakati wa ziara ya kikazi ya uhamasishaji wananchi kusalimisha silaha, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime amesema kumekuwa na mafanikio makubwa kuhusu suala hilo.

Akifafanua kuhusu mafanikio ya uwasilishaji silaha hizo, amesema yanatokana na elimu inayotolewa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo viongozi wa dini na kwamba Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa iliyofanya vizuri ,ambapo ilikusaya silaha 111 kati ya 1,220.

“Zoezi hilo limeonesha mwitikio mkubwa sana, ambapo Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa iliyofanya vizuri na tangu kampeni hii itangazwe tumefika Chalinze tayari wamekusanya sialaha za moto 11 …baada ya kukamilika kampeni ya awamu hii tutatoa taarifa ya takwimu zote kwa nchini nzima,”alisema Misime na kuongeza kuwa:

“Mwezi wa kampeni ya uwasilishaji silaha kwa hiari mwaka huu ilianza Septemba mosi na itamalizika Oktoba 31,2023 na kipindi hiki ndio kila mtu anayemiliki silaha kinyume na sheria anatakiwa kusalimisha kwa hiari na atakayefanya hivyo hatokamatwa wala kufunguliwa mashtaka …niwaombe wananchi kutumia frusa hii,”alisema.

Amesema silaha iliyokuwa inamilikiwa na mtu aliyefariki hairuhusiwi kutumiwa na mrithi wake, badala yake anapaswa kuiwasilisha polisi.

Amewataka Polisi Kata kushirikiana na viongozi mbalimbali walioko kwenye maeneo yao kuhamasisha wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kusalimisha silaha hizo kwa hiari.

 

Habari Zifananazo

Back to top button