Polisi wamuaga Sirro, azungumzia mauaji Kibiti

JESHI la Polisi Tanzania, limemuaga rasmi na kwa heshima zote Mkuu wa zamani wa Jeshi hilo (IGP) Simon Sirro, baada ya kustaafu utumishi ndani ya jeshi kwa mujibu wa sheria mwezi Machi mwaka huu, huku akisema matukio ya mauaji Kibiti ni miongoni mwa mambo ambayo hatayasahau.

Hafla hiyo ya kuagwa ambayo imefanyika Chuo Cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam imeongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini, ambapo Sirro alipigiwa gwaride maalum la kuagwa, huku akisukumwa kwa gari maalumu la Polisi.

Akizungumza baada ya hafla hiyo IGP Mstaafu Sirro, aliwashukuru Watanzania kwa ushirikiano mkubwa waliompatia kipindi cha uongozi wake na kwamba katika kipindi chake matukio ya mauaji ya Kibiti na uhalifu wa kutumia siraha, Panyaroad ni matukio ambayo hatayasahau.

Kwa upande wake IGP Camillus Wambura, pamoja na kumshukuru Sirro kwa kulijenga jeshi hilo, amesema kwa sasa wanaendelea kufanya mabadiliko, ili kuwa la kisasa na weledi zaidi, maadili na nidhamu kuanzia kwenye ajira, ili jamii ipate inachohitaji.

IGP Mstaafu Simon Sirro amelitumikia Jeshi la Polisi kwa kipindi cha miaka 30 tangu mwaka 1993 alipojiunga rasmi hadi kustaafu Machi mwaka huu na amekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi wa 10 tangu Uhuru na kwa sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe

Habari Zifananazo

Back to top button