Polisi wanawake kupelekwa nje ya nchi mwakani

JESHI la Polisi limejipanga kupeleka kikosi cha askari wanawake kati ya 120 hadi 150 kwa ajili ya kulinda amani Januari mwakani nje ya nchi ya Tanzania.

Kamishna wa Polisi Suzan Kaganda ameeleza hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 23 ya Maamuzi ya Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa jinsi unavyoweka kipaumbele cha mwanamke katika kudumisha amani.

Kaganda amesema Januari mwakani watapata timu kutoka Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kufanya tathmini hiyo ya kupeleka kikosi cha askari hao.

“Kwa hiyo tuna uhakika kwamba wakija wakifanya tathmini tutafaulu na tutapata mwaliko wa kupeleka kikosi. Uzuri wa kikosi tunachoaandaa asilimia 100 ya viongozi ni wanawake na tutakuwa na kikosi chenye askari wa kike,” amesema.

Amesema mara kwa mara amekuwa akishiriki kuona askari wa kike wanaongezeka kwa wingi zaidi, na kwamba mwaka 2019 Jeshi la Polisi kupitia tathmini inayofanywa na umoja wa mataifa walipata idadi kubwa ya askari wa kike kwa ajili ya kuwapeleka kushiriki kulinda amani.

“Changamoto kubwa tulionayo hususan kwa askari wetu ni moyo wa uthubutu na utayari kwa sababu ili kuweza kushiriki ulinzi wa amani askari wanapimwa vigezo mbalimbali ikiwemo kuendesha gari manual , kuzungumza kingereza na kujua matumizi ya silaha,” amesema.

Naye Mkuu wa Chuo cha Ulinzi wa Amani Tanzania, Brigedia Jenerali George Itang’are amesema azimio namba 1325 la baraza la usalama la umoja wa mataifa lililofikiwa mwaka 2000 lilikuwa na ajenda kuu moja la kuelezea wanawake, amani na usalama.

Lengo likiwa ni kuhakikisha kunakuwa na ushiriki bora kwa wanawake katika ulinzi wa amani.

“Kama chuo tuna program nyingi tunaendesha kwa lengo la kuongeza idadi ya walinzi wa amani wa kike. Tunachojivunia tuna idadi kubwa ya washiriki wanawake katika ulinzi wa amani nafasi za ukamanda na unadhimu,” amesema.

Amesema kunapokuwa hakuna amani waathirika wakubwa ni wanawake na watoto hivyo kwa kutumia wanawake wanafikia jamii kwa urahisi.

Kwa upande wake Mkuu wa Lugalo Hospitali, Meja jenerali Gabriel Mhidze amesema mwanamke ni muhimu katika kudumisha amani kwenye nchi zenye migogoro kwa sababu mama ndiye anaanzisha familia inayotengeneza jamii, hiyo familia kama itakuwa haina migogoro ndiyo itatengeneza nchi salama.

Amesema wakina mama wana mchango muhimu katika kudumisha amani kwenye nchi.

“Wanawake wanaweza katika ngazi mbalimbali katika taifa kuna viongozi kuanzia Rais, Mawaziri, Wabunge na idadi ya viongozi katika bunge imekuwa kubwa kuliko zamani na hata katika majeshi wanawake wameweza kupewa kipaumbele,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button