Polisi wasema kuna uzembe ajali ya mwendokasi

KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Muliro Jumnne Muliro, amesema ajali iliyotokea jana eneo la Kisutu jijini Dar es Salaam ilisababishwa na uzembe wa dereva wa gari ndogo, aina ya Toyota Avanza.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa  Dar es Salaam leo, Alhamisi Februari 23, 2023 imeeleza kuwa dereva huyo Jumbe Mohammed (38), hakuzingatia alama za barabarani hivyo kusababisha ajali hiyo.

“Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa chanzo cha ajali ni uzembe na kutojali alama za barabarani kwa dereva wa gari ndogo yenye namba T978 DHZ aina ya Toyota Avanza, aliyekuwa anatoka Mnazi mmoja kuelekea mzunguko wa DTV kutochukua tahadhari wakati anakatisha barabara kubwa ya Morogoro,” ACP Muliro alisema.

Jana basi la mwendo kasi liliacha njia na kugonga maduka katika eneo Kisutu, Dar es Salaam na kujeruhi watu kadhaa.

ACP Muliro aliongeza kuwa baadhi ya majeruhi waliokuwa wakipatiwa matibabu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili wameruhusiwa na wengine wanne wanaendelea na matibabu akiwemo, dereva wa Toyota Avanza, Jumbe Mohammed.

Majeruhi wengine wanaoendelea na matibabu ni, Shukuru Omari, Saidi Hasani na mtembea kwa miguu aliyetambulika kwa jina moja la Ismail.

Habari Zifananazo

Back to top button