JESHI la Polisi limetoa onyo kwa wananchi kujiepusha na kampuni zinazojinasibu na uwekezaji wa fedha kwa kuzichunguza kwanza na kujihakikishia kabla ya kuwekeza na kutapeliwa.
Aidha, limebainisha kuwa kutokana na malalamiko ya baadhi ya wananchi kutapeliwa fedha zao na kampuni ya Kalynda E Commerce kwa njia ya mtandao, Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kwa kushiriana na taasisi nyingine za kiuchunguzi na za kifedha wameanza kuchunguza malalamiko hayo ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Hayo yalielezwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime katika taarifa yake aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari.
Alisema wakati hatua hizo zikiendelea kuchukuliwa, jeshi hilo linatoa tahadhari tena kwa mara nyingine kwa Watanzania, kwani lilishawahi kuwatahadharisha huko nyuma wakati kampuni zingine ambazo ziliwahi kujinasibu kutoa huduma kama hizo, lakini waliojiingiza waliambulia kupoteza fedha na mali zao.
Alimtaka kila mmoja atambue kuwa kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani kote wahalifu wanatumia maendeleo hayo kupitia mitandaoni kutapeli mamilioni ya fedha kwa maneno ya kuvutia kuwa mtu atapata fedha nyingi katika kipindi kifupi kama atawekeza kiasi fulani cha fedha.
“Wengine wanajifanya kuuza bidhaa za aina mbalimbali au magari. Jambo la kujiuliza, kama hayo wanayokuvutia nayo ni ya kweli, kwa nini wasiwahamasishe ndugu zao na ukoo wao wakatajirika kama wanavyokudanganya? Hiyo huruma kwako wewe ambaye hamfahamiani inatoka wapi?” Alihoji Misime.
Alisema ni lazima kila mmoja atambue, kuna matapeli na usalama wa fedha au mali yake inaanza na yeye mwenyewe.
Aidha, alisema ni vyema kutambua hakuna utajiri au kujipatia fedha kwa njia rahisi kiasi hicho bila kutoka jasho kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi.
Alisema hata kama mtu amevutiwa kiasi na uwekezaji fedha kama wanavyotangaza mitandaoni, ni vyema kufanya utafiti kwanza, kwa kuuliza mamlaka zinazosimamia kupata ukweli.