Polisi watatu mbaroni wakidaiwa kupora mil 3/-

11 wadakwa gesti wakiwa nchini kinyemela

MAOFISA watatu wa Jeshi la Polisi mkoani Arusha akiwamo Mkuu wa Kituo cha Polisi Engutoto, Mkaguzi Msaidizi Mahamud Jakaya wamewekwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi kwa madai ya kumpora mfanyabiashara wa mazao kutoka Dodoma zaidi ya Sh milioni tatu.

Inadaiwa mfanyabiashara huyo Ramadhani Hamisi aliporwa fedha hizo Agosti 25, mwaka huu saa nne usiku baada ya kugoma kutoa rushwa ya Sh milioni 10 akituhumiwa kujihusisha na utumiaji wa mirungi.

Askari wengine waliokamatwa ni Mkaguzi Msaidizi Ramadhani Mcheka na Mkaguzi Msaidizi aliyetambulika kwa jina moja la Machanganya. Inadaiwa askari hao wapo Kitengo cha Polisi Jamii katika Wilaya ya Arusha.

Advertisement

Inadaiwa Hamisi alikamatwa eneo la Mrombo Mizani jijini hapa akiwa na ndugu zake wanne akiwamo dereva wake Nassibu Ngoyana wakiwa katika lori, wakapekuliwa na hakukuwa na mirungi.

Chanzo chetu cha habari kilidai kuwa baada ya upekuzi, Jakaya na Mcheka walimwamuru Hamisi ateremke na begi lake na akaingizwa kwenye gari dogo binafsi aina ya Porter lililokuwa likiendeshwa na Jakaya na alipelekwa katika Kituo cha Polisi Muriet.

Ilidaiwa kuwa askari hao wakiwa na mtuhumiwa hawakukaa kituoni hapo, waliondoka wakaenda Kituo Kikuu cha Polisi Arusha na njiani walipekua begi la Hamisi na kukuta Sh 7,100,000.

Chanzo kimedai askari hao walichukua Sh 30,000 bila ridhaa ya Hamisi na wakazitumia kununua mafuta ya gari.

Ilidaiwa askari hao walitaka rushwa ya Sh milioni 10, lakini Hamisi aligoma kutoa akisema hana kosa ila alikuwa tayari kuwapa Sh 300,000 kama ‘maji ya kunywa’.

Chanzo kilidai walipofika Kituo Kikuu cha Polisi, askari hao waliingia ndani na kumwacha Hamisi kwenye gari.

Ilidaiwa kuwa wakati wanaondoka katika kituo hicho walimweleza mfanyabiashara huyo kuwa wanachukua Sh 3,000,000 na afunge mdomo, na kwamba wangemwacha eneo la Kisongo arudi Dodoma.

Chanzo kilidai baada ya Hamisi kuachwa Kisongo, aliwasiliana na mjomba wake ambaye ni askari aliyetajwa kwa jina moja la Salehe na kumweleza mkasa uliompata.

Ilidaiwa Salehe aliwajulisha wakubwa zake na Agosti 26, asubuhi ilifanyika gwaride la utambuzi na mfanyabiashara huyo aliwatambua askari waliompora.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Justine Msejo alisema hana taarifa, na alipobanwa alisema alikuwa katika kikaokazi Moshi na alipotafutwa tena hakupokea simu.

Mfanyabiashara Hamisi alilieleza gazeti hili kuwa askari hao walimwomba rushwa ya Sh milioni 10 wakidai anajihusisha na utumiaji wa mirungi, tuhuma alizozikana.

Alidai kuwa askari hao walichukua fedha zake Sh 3,030,000 bila ridhaa yake na amekuwa akiitwa na askari wakubwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha (akiwataja majina), wakimtaka amalize kesi kwa kupewa Sh milioni 1.5, lakini amekataa.