Polisi yadaka 6 mauaji, kufukua makaburi

WATU sita wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Singida wakihusishwa na mauaji ya watu, ufukuaji wa makaburi na kuchukua viungo, baadhi ya vitu vya maiti katika maeneo tofauti wilayani Manyoni.

Imeelezwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida,  Stella Mutabihirwa, leo Machi 28, 2023 kuwa hatua hiyo imefuatia msako uliofanywa na Jeshi hilo, kati ya Machi 16 na 24 Mwaka huu.

“Msako ulifanyika kwenye maeneo tofauti ya Wilaya ya Manyoni na vijiji vya jirani vilivyo Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora,” amesema Kamanda Mutabihirwa.

Amesema katika mahojiano watuhumiwa hao wamekiri kuua mwanaume ambaye mwili wake ulikutwa kwenye eneo la reli, wilayani Manyoni Machi 3 mwaka huu.

RPC Singida,Stella Mutabihirwa

Akizungumzia tukio hilo,  Kamanda huyo amesema mwanaume huyo ambaye majina yake hayakufahamika, aliyekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 40 na 45, alikutwa akiwa amefariki na ikasadikiwa alikanyagwa na treni kichwani na mguu wa kushoto.

Amesema baadhi ya viungo vyake vilikutwa pembeni ya njia ya treni, kiwiliwili kilikutwa katikati ya njia ya treni, huku viungo vya sehemu zake za siri vikiwa vimenyofolewa.

“Watuhumiwa hawa wamesema wao ndiyo walihusika na kifo hicho, wamesema walikata sehemu ya siri, nywele, kucha na ulimi ili kutengenezea wateja wao dawa ya utajiri,” amesema Mutabihirwa.

Amesema katika kukamilisha upelelezi, jeshi hilo lilifanya upekuzi nyumbani kwa mmoja wa watuhumiwa hao ambako kulipatikana suruali nyeusi ambayo imebainika ilikuwa ya marehemu aliyepatikana Machi 3 mwaka huu relini Manyoni, vibuyu viwili vyenye shanga na kingine chenye ngozi ya kondoo.

Vitu vingine ambavyo vimetajwa naye kuwa vilikutwa kwenye nyumba hiyo ni pembe ya kondoo yenye kioo cha shanga, pembe ya ng’ombe yenye vipembe viwili vidogo, vipande vitatu vya sanda, kaniki vipande viwili, kitambaa kimoja chekundu na kopo la mafuta ya bodyluxe lenye mchanga wa makaburini na nywele.

Ametoa wito kwa wananchi, hususani wa Wilaya ya Manyoni, ambako kwa mujibu wake, vitendo vya ushirikina vinavyohusisha mauaji ya watu, ufukuaji wa makaburi na kuchukua viungo, vitu vya maiti vimekithiri kuacha imani hizo potofu kwa sababu mali hutokana na kufanya kazi kwa bidii na siyo vinginevyo.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x