Dereva bodaboda adaiwa kumuua mdai wake

JESHI la Polisi Mkoani Mtwara linamshikilia dereva wa bodaboda mkazi wa Kijiji cha Naipanga, wilayani Nachingwea, mkoani Lindi kwa tuhuma za mauaji ya Mwajuma Yusufu (32) pia mkazi wa Kijiji hicho.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Nicodemus Katembo, amesema tukio hilo lilitokea usiku wa Januari 4 kuamkia Januari 5 mwaka huu.

Amesema chanzo cha mauaji hayo ni kuwa marehemu Mwajuma alimkabidhi mtuhumiwa Sh 300,000, ili akamnunulie korosho kwa makubaliano ataziuza korosho hizo na kupata faida ya Sh 500,000.

Hata hivyo mtuhumiwa ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu upelelezi bado unaendelea, alimtumia marehemu Sh 40,000, kinyume cha makubaliano yao.

‘’Kutokana na kutotimiza ahadi waliyokubaliana, marehemu alimtaka mtuhumiwa waende sehemu alizopeleka korosho, ili kujiridhisha, lakini wakiwa njiani kuelekea maeneo hayo ambayo mtuhumiwa anadai alipeleka korosho, mtuhumiwa huyo alijifanya pikipiki imeishiwa mafuta, kisha waliposhuka akaanza kumshambulia kwa nondo, mawe hadi mauti,” alisema.

 

Habari Zifananazo

Back to top button