POLISI nchini kwa kushirikiana na wenzao wa nchini Malawi wamekamata watu wanne wakiwamo Watanzania watatu na Mmalawi wanaodaiwa kujihusisha na mtandao wa wizi wa magari katika nchi hizo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei Jumatano alitaja Watanzania waliokamatwa ni Yusuph Ramadhan (26) mkazi wa Forest jijini Mbeya, Shuku Nyema (23) mkazi wa Songea mkoani Ruvuma na Abuu Rutagalama (26) mkazi wa Itezi jijini Mbeya na raia wa Malawi, Richard Ng’oma maarufu kwa jina la Pinda (35).
Kamanda Matei alisema Aprili 4 mwaka huu saa 8 usiku katika mtaa wa Jelele uliopo katika Kata ya Itezi, Tarafa ya Sisimba, jijini Mbeya Ofisa Kilimo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Gidion Mapunda (45) aliibiwa gari lenye namba za usajili T 795 DEX aina ya Prado TX lenye rangi ya silver.
Alisema Julai 5 mwaka huu polisi walikamata watu watatu Watanzania na katika mahojiano walikiri kuhusika katika tukio hilo na kudai kuwa gari hilo walilisafirisha hadi Malawi na kumkabidhi Ng’oma.
Kamanda Matei alisema Agosti 31 hadi Septemba 2 mwaka huu polisi wa Mbeya walifika Malawi na kushirikiana na wa Malawi wakamkamata Ng’oma akiwa na gari hilo na alikiri kulipokea kutoka kwa Omary.
Alisema siku hiyo hiyo Ng’oma alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kalonga nchini humo na kutolewa ushahidi na mmiliki wa gari, Mapunda na mtuhumiwa, Yusuph Omary.
Kamanda Matei alisema baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi uliotolewa ilimtia hatiani Ng’oma na kukabidhi gari hilo kwa Jeshi la Polisi Tanzania kwa ajili ya taratibu za kumrejeshea mmiliki.
Alisema polisi mkoani Mbeya wanaendelea na utaratibu wa kisheria kuwafikisha mahakamani watuhumiwa Watanzania.
Kamanda Matei alisema jeshi hilo pia linamshikilia mkazi wa Kitongoji cha Chikula katika Kijiji na Kata ya Ifumbo, Tarafa ya Kiwanja, wilayani Chunya, Mabula Mabhembe (35) kwa tuhuma za kuuza bangi dukani kwake.
Alisema Male alikamatwa Septemba 5 mwaka huu saa 11 jioni katika duka lake la bidhaa za nyumbani akiwa na magunia matatu ya bangi yenye uzito wa kilogramu 20, misokoto 3,500 na rizla maboksi mawili.