JESHI la Polisi mkoani Geita limeiomba serikali kuitazama mada ya ukatili wa kijinsia kuwa sehemu ya mitaala ya kufundishia kwenye shule za msingi ili kuwaandaa watoto kukabiliana na vitendo vya ukatili.
Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Berthaneema Mlay ametoa mapendekezo hayo Aprili 14, 2023 kwa niaba ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita katika hafla ya kuhitimisha mashindano ya polisi jamii wilayani Chato.
Hitimisho la mashindano hayo lilichagizwa na umoja wa maaskari wanawake Geita kutembelea shule ya watoto yatima Binghamm, gereza la Chato na hospitali ya wilaya Chato na kutoa misaada mbalimbali.
ACP Berthaneema amesema ili kushinda vita dhidi ya ukatili wa kingono na kijinsia kwa watoto wa kike na wa kiume, watoto wote wanapaswa kung’amua maana halisi ya ukatili toka wakiwa wadogo.
Ameeleza, kupitia mada hiyo watoto watajifunza na kuelewa maeneo ya mwili ya kuyalinda na kuyatunza wenyewe pasipo kuruhusu mtu yeyote awashike na kuwachezea na hivo kuimarisha ulinzi wa miili yao.
“Mtoto akijua kitu hiki ni kibaya na kitu hiki ni kizuri itamusaidia yeye kusema hapana pale ambapo anakumbana na kile kibaya au anaposhawishiwa kufanya yale ambayo hayafai.
“Kuingiza hiyo mada ya ukatili wa kijinsia kwenye masomo yao na kuwafundisha wanafunzi kinagaubaga na ukweli halisis wasifiche chochote wajue jamii inaendaje, itasaidia watoto kuwa salama zaidi.”
Amesema kuwaficha watoto haisaidii kwani inawaweka kwenye mazingira ya kudanganywa kwa urahisi na ndugu ama wanafamilia ambao kwa siku za hivi karibuni wameripotiwa sana kufanya vitendo vya ukatili.
“Nawasihi pia na walimu, kuanzia shule za msingi, sekondari hata vyuo wajitahidi kulea wale watoto kama watoto wao ajitahidi kufikiria, je angekuwa ni mtoto wangu anafanyiwa hivi vitendo ningevumilia.”
Meneja wa Shule ya watoto yatima ya Binghamm Chato, Naseeb Yassin amekiri kwa kufungamanisha mada ya ukatili wa kijinsia na masomo ya dini ni wazi kwamba watoto watakuwa mabalozi wazuri kukomesha ukatili wa kijinsia.